Kampuni kubwa ya biashara ya utalii duniani kupitia mtandao Expedia Group, imeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Bodi ya Utalii (TTB) kutangaza na kuleta watalii wengi zaidi Tanzania.
Kauli hiyo imetolewa mjini Seattle nchini Marekani na Mkurugenzi Mwandamizi wa Masoko ya Kimataifa wa kampuni hiyo. Andrew Van Der Feltz, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi.
Kwa upande wake Dkt. Abbasi aliyefuatana na Mtendaji Mkuu wa TTB, Damasi Mfugale, amewahakikishia watendaji hao wa Expedia kuwa Tanzania kwa sasa imeamua kuja na mtazamo mpya katika kutangaza utalii.
“Tunaamini utaalamu wenu na uzoefu wenu katika masoko na biashara ya utalii kimtandao utasaidia kuongezea juhudi za Rais wetu wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amefanya juhudi kubwa kupitia filamu ya Tanzania; The Royal Tour kuiweka Tanzania katika taswira pana zaidi kimataifa katika utalii na uwekezaji.” Amesema Dkt. Abbasi
Expedia ni kampuni inayotumia teknolojia za kisasa katika kutangaza na kuhudumia watu zaidi ya Milioni 400 kwa mwezi duniani, inatumia muunganiko wa zaidi ya tovuti 200 na inafanya kazi na mashirika ya ndege na wabia wengine zaidi ya 500.
Inashika nafasi ya pili duniani na imewahi kushika nafasi ya kwanza nchini Marekani kwa kuaminiwa na watalii katika sekta ya usafiri na utalii.