BENKI ya Exim imetangaza kupata faida ya Sh bilioni 25.3 kabla ya kodi kwa mwaka 2020 ikilinganishwa na hasara ya Sh bilioni 8.4 iliyopata mwaka 2019, hali inayoakisi ukuaji wa asilimia 402 wa mwaka hadi mwaka.
Mafanikio hayo yanayotajwa kuwa yametokana na ufanisi wa kiutendaji licha ya changamoto za kiuchumi kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa covid-19 ulioathiri ukuaji wa uchumi katika baadhi ya sekta muhimu nchini mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa wa benki hiyo, Jaffari Matundu jijini Dar es Salaam jana, benki hiyo imetekeleza kwa ufanisi mkubwa mkakati wa kushirikiana na sekta zinazofanya vizuri sambamba na kuongeza umakini katika matumizi yake ili kuongeza tija zaidi.
“Katika kipindi hicho benki ilikuwa bega kwa bega na sekta zilizoathiriwa na janga hilo na kwa kweli tulishirikiana kikamilifu na wateja wetu kuhakikisha si tu tunawapatia fedha, bali pia tunawajengea uwezo wa kufanya shughuli zao katika kipindi hicho kigumu,’’ alisema.
Matundu alisema hadi kufikia Desemba 31, mwaka jana, benki hiyo ilikuwa imetoa msamaha wa zaidi ya Sh bilioni 290 kwa njia ya likizo ya malipo na upanuzi wa vipindi vya ulipaji wa mikopo ili kusaidia wateja wake ambao biashara zao ziliathiriwa zaidi kiuchumi na covid-19.
"Tumefanikiwa kurejesha asilimia 9.0 ya faida kwenye mfuko wa wanahisa ikilinganishwa na marejesho hasi ya asilimia 9.2 mwaka 2019," alisema Matundu.
Alisema nchini benki hiyo ilirekodi mafanikio kwa kupata faida kabla ya kodi ya Sh bilioni 18.8 kutoka kwenye hasara ya Sh bilioni 14.5 kabla ya kodi ya mwaka 2019.
"Mafanikio hayo yamechangiwa na kuongezeka kwa mali kutokana na usafishaji uliofanywa katika kipindi hicho cha mwaka uliopita hatua iliyosababisha kupungua kwa mikopo chechefu kutoka asilimia 22.3 ya mwaka 2019 hadi asilimia 7.4 mwaka 2020.”
"Matawi yetu ya nchini Djibouti na Comoro pia yalirekodi faida ya Sh bilioni 4.9 na Sh bilioni 5.7 kabla ya kodi licha ya athari ya covid-19.”
“Jumla ya mali zetu imebaki kuwa Sh trilioni 1.9. Amana za wateja zimeongezeka kwa asilimia 4.4 wakati wa robo ya mwaka na kufikia Sh trilioni 1.38. Shughuli zetu nchini Tanzania, Comoro na Uganda zote zimerekodi ukuaji wa ajabu katika amana za wateja wakati wa robo ya mwisho wa mwaka,” alisema.
Alisema mafanikio hayo kwa kiasi kikubwa yanachochewa na kauli mbiu ya benki hiyo ya ‘Exim kazini leo kwa ajili ya kesho' ambayo imekuwa ikiisukuma benki hiyo kubuni huduma mpya zinazoendana na mahitaji ya wateja wake.