Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Exim, ZATI wasaini makubaliano kukuza utalii Zanzibar

Extension To Zanzibar Exim, ZATI wasaini makubaliano kukuza utalii Zanzibar

Mon, 28 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Benki ya Exim Tanzania na Jumuiya ya Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI) wameingia makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji hatua inayolenga kuinua kuboresha utoaji wa taarifa kwa sekta ya utalii visiwani hapa.

Ushirikiano huo unatoa fursa kwa wadau hao kushirikiana kuhakikisha taarifa zote muhimu kuhusu utalii visiwani hapa zinapatikana kwa urahisi duniani kote na wanachama wa ZATI wanapata ufumbuzi wa mahitaji yao.

Akizungumza wakati hafla fupi ya utiaji saini makubaliano hayo yaliyofanyika Machi 25 visiwani hapa, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohamed pamoja na kuwapongeza wadau hao ameyataja makubaliano hayo kuwa ni ya kipekee.

Amesema hatua hiyo inakwenda sambamba na azma ya Serikali ya kuimarisha ushirikiano miongoni mwa taasisi za sekta binafsi pamoja mahusiano baina ya serikali na sekta binafsi.

“Ni imani yangu uhusiano huu mzuri baina ya wadau wa Serikali na taasisi za kifedha utasaidia kuinua utalii Zanzibar ambao umeathiriwa sana na Uviko-19.

“Wadau wa utalii sasa watajikwamua na kurejesha uwezo wao wa kiuchumi. Natoa wito kwa taasisi nyingine za fedha kuiga mfano huu kwa kuwa karibu na wadau wa utalii hasa katika zama hizi ambapo Serikali inajikita zaidi katika uchumi wa bluu,” amesema.

Utalii unachangia takribani 25 asilimia ya pato la Taifa visiwani Zanzibar na hadi asilimia 80 ya mapato ya fedha za kigeni.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Jaffari Matundu amesisitiza kuwa hatua hiyo ni muendelezo wa mkakati wa benki hiyo kuendelea kukuza sekta ya Utalii nchini.

"Sekta hii muhimu ya utalii ni moja ya sehemu ambayo tunaitazama zaidi hasa visiwani Zanzibar na maeneo mengine hapa nchini hivyo, naahidi tutaendelea kujidhatiti zaidi hilo. Utalii ni nguzo muhimu ya uchumi wetu na sisi tutaendelea kuzingatia hilo kwa kuwekeza zaidi,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya miaka mitatu, benki hiyo itahusika katika kuhakikisha wadau wa utalii wanapata mikopo ya biashara kubwa na ndogo inayoandaliwa kulingana na mtiririko wa fedha za mwanachama husika.

Naye Mwenyekiti wa ZATI, Rahim Bhaloo ameipongeza Exim kwa ushirikiano huo na kusema hatua hiyo itaiwezesha sekta ya kimkakati ya utalii kuongeza kasi, kuinua ubora wa huduma na kuongeza mvuto wa visiwa hivyo kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.

“Ni muhimu kueleza hatua hii ni matokeo ya ushirikiano na wenye tija kati ya ZATI na wadau wakiwemo wanachama wake, taasisi za fedha. Ushirikiano huu huu utatuwezesha kusaidia ipasavyo biashara yetu ya utalii, kutengeneza ajira, na kuboresha ustawi wa wawekezaji wadogo na wakubwa katika sekta ya utalii,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live