Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ewura yatoa gawio bil 68/- miaka saba

Fb71f8ce378cd6e45cc12205f0d3f244.jpeg Ewura yatoa gawio bil 68/- miaka saba

Thu, 4 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imechangia gawio la Sh bilioni 67.6 kwenye mfuko wa serikali kupitia kwa Msajili wa Hazina katika kipindi cha miaka saba (2012-2019).

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje, aliyasema hayo jana jijini Mwanza wakati akizungumza kwenye semina ya siku moja na waandishi wa habari wa mkoani Mwanza.

Chibulunje alisema mchango huo wa gawio serikalini ulichangiwa na mamlaka za udhibiti zilizo chini yake likiwemo Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Nishati (Ewura CCC) lililochangia Sh bilioni 12.

Alisema, Baraza la Ushindani wa Haki katika Biashara (FCC) lilichangia Sh bilioni 4.7, Baraza la Ushindani (FCT) Sh bilioni 2.7, na Baraza la Ushauri la Serikali (GCC) lilichangia Sh milioni 905.

Kuhusu ubora wa mafuta, Chibulunje alisema Ewura imepambana na changamoto ya uchakachuaji wa mafuta hivyo tatizo limepungua kutoka asilimia 80 mwaka 2007 hadi asilimia nne mwaka 2020.

Alisema hatua hiyo ilifikiwa baada ya Ewura Septemba 2010 kuanzisha programu ya kuweka vinasaba kwenye mafuta yanayotumika nchini kwa lengo la kudhibiti ukwepaji wa kodi na uchakachuaji.

Chibulunje alisema Ewura imeandaa mfumo wa uuzaji mafuta vijijini kwa kutumia vituo vinavyotembea ili kuongeza upatikanaji wa mafuta kwa njia salama na zinazozingatia utunzaji mazingira.

Kuhusu udhibiti wa bei za mafuta, Chibulunje alisema baada ya EWURA kuona bei za mafuta zinapanda kiholela iliingilia kati kwa kuanza kutoa bei kikomo.

Alisema utafiti uliowahi kufanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ulianisha kuwa udhibiti wa bei za mafuta umefanikisha kukua kwa pato la ziada la wananchi kwa kiasi cha Sh bilioni 445.5 kati ya mwaka 2009 na 2010.

"Udhibiti huo wa bei za mafuta nchini umechangia katika kuongeza mapato ya kodi ya Serikali kwa Sh bilioni 49 kwa kipindi cha mwaka 2009 hadi Juni 2010," alisema.

Kuhusu uagizaji wa mafuta nje ya nchi kwa mfumo wa uagizaji wa pamoja wa mafuta (BPS), alisema utafiti uliofanywa na UDSM April 2014, ulibaini kuwa mfumo umesaidia kupunguza gharama ya Sh bilioni 121.57 kwa mwaka.

Alizitaja gharama zilizopunguzwa kuwa ni pamoja na za usafirishaji kwa kiasi cha Sh bilioni 81.90 kwa mwaka, gharama ya upakiaji wa mafuta kwenye meli kabla na baada ya kupakia mafuta kwa Sh bilioni 25.72 kwa mwaka na gharama za uagizaji mafuta kutokana na maboresho ya mikataba kwa Sh bilioni 13.95 kwa mwaka.

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko, aliushukuru uongozi wa Ewura kwa kukubali kuandaa mafunzo kwa wandishi wa habari kutoka mikoa ya Mara, Shinyanga, Simiyu na Mwanza yaliyowajengea uwezo wa kuifahamu mamlaka hiyo.

Chanzo: habarileo.co.tz