Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ewura kuanzisha uuzaji mafuta vijijini kwa kirikuu

46206 PIC+EWURA Ewura kuanzisha uuzaji mafuta vijijini kwa kirikuu

Tue, 12 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wakati majeruhi wa mwisho wa kulipukiwa na moto wa petroli wilayani Same akifariki dunia na kufanya idadi kufikia saba, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishaji na Maji (Ewura), itarekebisha kanuni zake ili kuruhusu uuzaji wa mafuta vijijini kwa gari ndogo za mizigo na pikipiki.

Aliyefariki juzi katika Hospitali ya KCMC ni Yusuph Sudi (10), mtoto wa muuguzi wa Zahanati ya Kijiji cha Marwa, Christina Mndeme ambaye naye alikufa katika ajali hiyo.

Moto huo ulilipuka katika nyumba moja Kijiji cha Marwa, Same, wakati muuguzi huyo akimpimia mafuta mteja jirani na jiko la mkaa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah, alisema jana kwamba kutokana na kifo hicho, majeruhi wote saba wa janga hilo wawe wamepoteza maisha.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Marwa, Elifuraha Masoni alisema Sudi anatarajiwa kuzikwa Arusha leo.

Alisema tukio hilo limeibua hofu kijiji kwake na wananchi wameanza kuchukua tahadhari kupinga uuzaji wa petroli nyumbani.

Alisema ipo haja kwa Serikali kutoa elimu ya madhara ya kuuza petroli kienyeji akisema maeneo mengi vijijini yanatumia mfumo huo.

Mkakati wa Ewura

Akizungumzia matukio hayo, Meneja Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo alisema, “kwanza tumerekebisha kanuni za ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini kutoka mwekezaji kuwa na kati ya Sh400 milioni hadi Sh1 bilioni ili kijijini mwekezaji aweze kuwekeza hata kwa Sh50 milioni.

“Kwa kupunguza mashariti ya gharama za ujenzi watu wengi watawekeza vijijini. Lakini la pili ni kwamba Ewura imemtafuta mtaalamu mwelekezi ili kutengeneza vituo vya kutembea (mobile).

Alisema mtaalamu huyo mwelekezi, taasisi ya BICO kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) itakuja na mfumo wa namna vituo hivyo vitasaidia kuepusha majanga ya moto.

“Mfumo unaopendekezwa utakuwa ni tenki dogo la mafuta kuwekwa kwenye vigari vidogo kama kirikuu au pikipiki ya magurudumu matatu, ambazo zitajaza mafuta sema lita 100 au 50, alisema Kaguo.

“Hawa sasa ndio wataruhusiwa kuuza mafuta maeneo ya vijijini tu. Mfumo huo bado upo hatua za awali... Tunashauri wakati tunangojea mfumo huo tuwe makini na uuzwaji wa mafuta kiholela kwenye maduka ya bidhaa za vyakula kwa usalama wa maisha yetu. Tuyalinde kuliko kitu chochote.

Tamko la polisi

Kutokana na tukio hilo la mlipuko wa petroli, Kamanda Issah amewataka wananchi kuacha kuhifadhi mafuta hayo ndani kwa kuwa ni hatari kwa maisha yao.

Alisema jeshi hilo litaendesha msako katika kata hiyo na mtu atakayebainika kuweka petroli ndani atakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Kama hatari imeshawapata wenzetu, watu wachukue tahadhari, waache kabisa kuhifadhi petroli ndani ya nyumba.

“Huyu alihifadhi petroli dumu mbili za lita 20. Moto umelipuka kusababisha vifo vya watu saba wengine wakiwa watoto wadogo sasa watambue petroli inahifadhiwa kwenye vituo vya mafuta na si ndani ya nyumba,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz