Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ewura inavyodhibiti majanga ya moto biashara ya mafuta

Mafuta Ya Petrol (1) Ewura inavyodhibiti majanga ya moto biashara ya mafuta

Thu, 15 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Agosti 10, 2019, Tanzania ilipoteza zaidi ya watu 70 kwa ajali ya moto wa malori ya mafuta. Ajali hiyo ilitokana na kupinduka kwa lori la mafuta karibu na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu, Morogoro.

Lori hilo lilipinduka baada ya dereva kumkwepa mwendesha pikipiki na mafuta yaliyomwagika kushika moto na kuunguza walioenda kuyachota.

Ni miaka mitatu imepita tangu ajali hiyo itokee, machungu yamepoa lakini athari zake na nyingine kama hizo zinazotokea nchini zinaendelea kuonekana katika jamii hivyo kuhitaji hatua kuzuia.

Kwa kutambua wajibu wake katika kuzuia ajali hizo zisitokee na hata zikitokea madhara yake yasiwe makubwa kama ajali ya Morogoro na ile ya Mbeya iliyoua wengi miaka ya 90, Mamlaka ya Udhibiti Nishati na Maji (EWURA) imeanza kutoa elimu.

Meneja Mawasiliano kwa Umma Ewura, Titus Kaguo anasema wanatoa elimu kwa wananchi kuepuka kukimbilia maeneo ya ajali za malori au visima vya mafuta ili kudhibiti matukio ya vifo vya watu na uharibifu mali utokanao na moto.

Kwa wanaofuatilia mashindano ya Kombe la Dunia yanayoendelea nchini Qatar hivi sasa, watakuwa wamesikia tangazo la Ewura la elimu kwa umma kuhusu ajali ya moto utokanao na malori ya mafuta ikitaka wasikimbilie eneo la ajali bali watoe taarifa.

Ni wazi, kwa kutoa elimu hiyo kwa umma kupitia Kombe la Dunia ambalo linatazamwa katika televisheni na kusikilizwa katika redio mbalimbali zikiwemo za jamii kama Ebony ya Iringa inayorusha tangazo hilo, Ewura imefanikiwa kuwafikia mamilioni ya watu.

Kaguo anasema, lengo la Ewura ni kudhibiti kwa kiwango cha juu ajali za moto ya malori ya mafuta au visima vya mafuta ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao ikiwa ni kutekeleza dhima yake kuu ya usimamizi na udhibiti wa sekta hiyo.

Kwa mujibu wa tovuti ya Ewura, kuna visima vya mafuta zaidi ya 2,500 nchini na maghala makubwa na madogo ya hifadhi za mafuta Dar es Salaam na mikoani. Kutokana na ukosefu wa bomba la kusafirisha mafuta (ukiacha la Tazama la Tanzania na Zambia), nishati hiyo husafirishwa kwa malori kutoka bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara kwenda mikoani na nchi jirani za Congo DR, Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda, Uganda.

Kaguo anasema usafirishaji huo kwa kutumia malori una changamoto kadhaa moja ikiwa hiyo ya malori kupata ajali na kuwaka moto hivyo kulazimu Ewura itoe elimu kwa umma kudhibiti ajali za moto.

Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Billy Mwakatage anasema gari lolote likianguka na shehena ya mafuta halipaswi kukaribiwa; mtu asiye mtaalamu hapaswi kulisogelea, na si mafuta tu bali pia bidhaa nyingine zinazosafirishwa na vyombo vya usafirishaji kama sumu pamoja na kemikali hatari.

Anasema sasa hivi kuna mfumo wa utoaji elimu kuhusu namna ya kupambana na majanga ya moto, elimu inayotolewa kwenye shule mbalimbali nchini.

”Jeshi la Zimamoto limepita kwenye shule za msingi na sekondari kuwafundisha. Tumeanzisha fire clubs zinazofundisha namna ya kuchukua tahadhari wakati wa majanga ya moto ili waelewe madhara ya moto pia tahadhari za kuchukua kujilinda nao,” anasema.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza la BBC, si mara ya kwanza matukio ya malori yaliyobeba mafuta kuwaka moto Afrika Mashariki na Kati. Mwaka 2010, watu 292 walifariki dunia Congo DR na 2015 watu 203 walifariki Sudan Kusini.

Ukiacha ajali za moto za malori ya mafuta, mara chache pia hutokea ajali za visima vya mafuta. Hivi karibuni, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula alisitisha utoaji wa vibali vya ardhi kujenga visima vya mafuta ili sheria mipango miji ifuatwe kulinda usalama wa watu.

Baadhi ya wafanyabiashara wasiozingatia usalama wamekuwa wakinunua maeneo ya makazi ya watu na kuyageuza maeneo ya visima vya mafuta bila kufuata sheria za mipango miji na kuhatarisha maisha ya wakazi wa maeneo visima vinakojengwa.

Wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakishirikiana na maofisa ardhi kubadili ramani za mipango miji kwa kununua makazi ya watu na kuyabadili kiholela kuwa visima vya mafuta hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi kunapotokea janga la moto. Sheria inataka nafasi ya mita 500 iachwe.

Kwa kutambua wajibu wake kulinda usalama wa wananchi dhidi ya majanga ya moto yatokanayo na biashara ya mafuta, Kaguo anasema Ewura inataka wafanyabiashara na wenye vyombo vya moto kuhifadhi mafuta katika miundombinu sahihi ili kuepuka ajali za moto za malori au visima hivyo.

Meneja wa Ewura Kanda ya Kaskazini, Lorivii Long’idu alisema katika semina maalumu ya kuwapa uelewa wa majukumu yao, watendaji wa kata, mitaa na vijiji, maofisa biashara na waandishi wa habari wilayani Babati mkoani Manyara, Ewura inasisitiza ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta katika maeneo ya vijijini na kuachana na mbinu za kienyeji za kuhifadhi mafuta kwenye makopo (chupa) ili kuepuka ajali zitokanazo na milipuko ya mafuta ambayo hayajahifadhiwa kitaalamu inavyotakiwa.

Alisema, Ewura imetoa leseni 1,561 za biashara ya mafuta zikiwemo za biashara ya mafuta ya jumla 66, ya rejareja 1,397 na leseni 19 za gesi ya kupikia na vilainishi vya mitambo 56 na kuwataka wafanyabiashara hao kuzingatia usalama.

Alieleza Ewura ipo kwenye mpango wa kuanzisha vituo vya mafuta vinavyotembea kukabili upungufu wa mafuta maeneo yasiyo na vituo vikubwa vijijini. Imedhibiti uchakachuaji kutoka asilimia 74 mwaka 2007 na hadi asilimia nne tu kufikia mwaka 2019.

Je, Ewura kutoa elimu kwa umma kutasaidia kudhibiti majanga? Jibu ni ndio. Kaguo anasema, ndio kwanza wameanza na watendaji waliopata elimu hiyo Babati waliahidi kuitoa kwa wananchi ili kuwajengea uwezo wajue huduma inazotoa Ewura.

Mbali ya kusimamia na kudhibiti nishati, mamlaka pia inahusika na maji safi na usafi wa mazingira. Imetoa leseni 24 za daraja la tatu za miaka10 kwa mamlaka za makao makuu ya mikoa na leseni 81 kwa zile za miji ya wilaya, midogo na miradi ya maji ya kitaifa.

Hata hivyo, Ewura inakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo gharama kubwa za uendeshaji kutokana na kufanya kazi ya kudhibiti mamlaka 13 za maji, ambapo kati ya hizo 95 ni za wilaya na miji midogo zenye wateja kati ya 4,000 na 50,000.

Ili kumudu huduma, inashirikiana na Wizara ya Maji na Tamisemi kuzijengea uwezo na kuangalia uwezekano kuunganisha taasisi ndogo na kubwa za miji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live