Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Eneo nyeti kwa kukuza uchumi

Uchumi Wa Buluu Eneo nyeti kwa kukuza uchumi

Tue, 18 Apr 2023 Chanzo: mwanachidigital

Wakati Shirika la Fedha Dunia (IMF) limetoa taarifa inayoonyesha pato la Tanzania (GDP) limepanda hadi kufikia Dola bilioni 85.42 (Sh199.47Trilioni) huku pato la mtu mmoja mmoja likitajwa kufikia Dola 1,350 (Sh3.15milioni), wachumi wameshauri uwekezaji ufanyike katika sekta ya kilimo ili mwananchi apate ahueni ya maisha.

Wanasema ili ukuaji huo uakisi maendeleo ya watu kuna haja ya kuongeza nguvu zaidi katika kukuza sekta zilizoajiri watu wengi hasa kilimo kinachotegemewa na zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania.

Ushauri huo wa wachumi unakuja huku makisio ya IMF yakionyesha kuwa kwa mwenendo uliopo hadi mwaka 2028 Tanzania kutakuwa na watu milioni 73.36, pato la Tanzania litakuwa dola bilioni 136.09 (Sh318.8 trilioni) na pato la mtu mmoja mmoja litakuwa dola 1,860 Sh4.3milioni) huku mfumuko wa bei ukiwa asilimia 3.7 na kasi ya ukuaji wa uchumi itakuwa asilimia 7.

Akizungumza na Mwananchi, kuhusu ripoti hiyo, Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo kikuu cha Dodoma, Dk Mwinuka Lutengano alisema ongezeko hilo linatokana na hatua zilizochukua na Serikali miaka ya hivi karibuni ambazo zilitoa fursa ya kukua kwa uchumi licha baadhi ya mataifa kuwa na ukuaji hasi.

“Kwanza namna tulivyoishi wakati wa mlipuko wa Uviko-19 hatukusitisha shughuli zetu hivyo uchumi uliendelea kukua lakini pia licha ya changamoto hiyo na nyingine zilizofuatia ikiwemo ya vita vya Ukraine Serikali yetu imeendelea kufungua nchi zaidi na kukaribisha uwekezaji wa ndani ambao ni muhimu sana katika ukuzaji wa uchumi,” alisema Dk Lutengano.

Mtaalamu mwingine wa Uchumi, Dk Donath Olomi yeye alisema kuongezeka kwa GDP ni habari njema lakini imechangiwa zaidi na miradi mikubwa inayojengwa kwa mikopo, hivyo ingefaa zaidi kama ingekuwa ni ukuaji wa sekta ambayo imeajiri watu wengi au kutumia miundombinu hiyo kuzalisha zaidi.

“Kama umejenga majumba makubwa kwa mkopo, ukiandaa hesabu za mali ulizo nazo lazima zionekane imeongezeka sana. Na utajiri huo utakuwa na maana kama utatumia mali ulizopata kwa mkopo kuongeza kasi ya kuzalisha ili uwe na uwezo wa kurejesha kulipia hizo mali,” alisema.

Dk Olomi, alisema kuna manufaa mengi ya ongezeko hilo kwani kuongezeka GDP kwa kawaida kunaambatana na kuongezeka uwezo wa uzalishaji, kuzalisha ajira, mapato ya Serikali na hivyo huduma kwa jamii huimarika.

Kutokana na ripoti hiyo wapo wanaomtazama Rais Samia kama mtu aliyebadili mchezo katika masuala ya uchumi na fedha licha ya kuwa alichukua uongozi katika kipindi kigumu ambacho uchumi wa mataifa mbalimbali ulikuwa kwenye msukosuko kutokana na athari za Uviko-19 na vita vya Russia na Ukraine.

Waziri wa fedha, Dk Mwigulu Nchemba aliliambia Mwananchi, kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita makisio ya kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania yamekuwa hayafikiwi kwa sababu ya mambo matatu likiwemo suala la vita kati ya Russia na Ukraine.

“Tumekuwa na mipango yetu na makisio ya ukuaji wa uchumi lakini yamekuwa hayafikiwi sababu ya mlipuko wa Uviko-19, mabadiliko ya Tabia ya nchi na Vita vya Urusi na Ukraine, Wakati tunaanza kupata ahueni kutoka kwenye Uviko-19 vita navyo vikaanza lakini yote hayo yanatupa somo la kujitoshelezea mahitaji yetu ya ndani na ndiyo mwelekeo wa Serikali,” alisema.

Kwa mujibu wa IMF kuongezeka kwa pato la Taifa sasa kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya sita kwa uchumi kati ya mataifa ya kusini mwa jangwa la sahara ikizipita Ivory Coast na Ghana ambazo awali zilikuwa juu yake, katika orodha hiyo Nigeria bado inaongoza kwa uchumi mkubwa Afrika pato lake likiwa ni Dola bilioni 506.6.

Vilevile thamani ya fedha zinazozunguka mikononi mwa watu Machi 2021 zilikuwa Sh4.2 trilioni lakini zilizokuwa mikono mwa watu Januari 2023 ilikuwa Sh5.29 trilioni jambo ambalo linaashiria vyuma kulegea.

Kadhali katika kipindi cha miaka miwili makusanyo ya kodi ambapo katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/23 TRA imekusanya Sh12.4 trilioni (Julai hadi Desemba 2022) kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa kwa kipindi cha nusu mwaka.

Kwa kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali chini ya Rais wa awamu ya tano ilikusanya Sh10.10 trilioni.

Kwa upande wa mfumko wa bei mpaka Januari 2023 uchumi ulikuwa kwa kiwango cha asilimia 4.8 wakati Machi, 2021 wakati Samia akichukua nchi ulikuwa asilimia 3.3.

Hata hivyo ikilinganisha na mataifa mengine, bado Tanzania kuna kiwango kidogo cha mfumko wa bei taifa kama Zimbabwe mfumko wake wa bei ni asilimia 92.8, Sudani 83.6 na Ghana ni asilimia 52.8, Mataifa mawili ya Afrika Mashariki (Burudi na Rwanda) yana asilimia zaidi ya 28.

Dondoo

Kutokana na taarifa hiyo mpya ya IMF Ukanda wa Afrika Mashariki unatoa nchi tano katika orodha ya nchi 10 zenye uchumi mkubwa barani Afrika, Ethiopia yenye uchumi wa dola bilioni 156 inaongoza katika ukanda na ikishika nafasi ya tatu Afrika, Kenya Dola bilioni 118.1 nafasi ya 4 Afrika, Tanzania Bilioni 85.4 nafasi ya sita, DRC bilioni 69.4 nafasi ya 8 na Uganda bilioni 49.7 nafasi ya 10.

Chanzo: mwanachidigital