Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Eneo la kiwanda cha General Tyre kubadilishwa

Mkumbo WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo

Tue, 17 Aug 2021 Chanzo: ippmedia.com

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo, amesema serikali ipo katika mchakato wa kubadilisha eneo la kiwanda cha matairi cha General Tyre, kuwa mtaa wa viwanda.

Uamuzi huo unatokana na kiwanda hicho kutokidhi mahitaji ya kuendelea kufanya uzalishaji wa matairi, kulingana na teknolojia na uhitaji wa soko.   “Tunaamini kama wizara, kwamba eneo hili litachochea maendeleo ya nchi. Kiwanda cha General Tyre kilichoacha kufanya uzalishaji kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita kutokana na teknolojia ya uzalishaji kupitwa na wakati.

“Lakini matairi yaliyokuwa yanazalishwa kukosa soko. Lengo la kufanya eneo hili kuwa mtaa wa viwanda ni kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuleta ajira kwa Watanzania hasa watu wa Arusha.”   “Serikali ipo katika mchakato wa kubadilisha eneo la Kiwanda cha Matairi cha General Tyre kilichoko Arusha kuwa Mtaa wa Viwanda ‘Industrial Park’ kutokana na kiwanda hicho kutokidhi mahitaji ya kuendelea kufanya uzalishaji wa matairi kulingana na teknolojia na uhitaji wa soko,” alisema.   Vilevile, Prof. Mkumbo alisema kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara ipo katika mchakato wa kuanzisha mitaa ya viwanda nchi nzima na tayari imeanza kwa kuchagua maeneo machache.   Maeneo hayo yataanzishwa mitaa mikubwa ya viwanda itakayoweza kuleta tija nchi nzima na kuchochea uchumi.   Kwa mujibu wa waziri huyo, mitaa hiyo itaanzishwa katika mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Kilimanjaro, Mwanza na Arusha, ambapo pia kuna timu inaendelea kufanya utafiti kwenye mikoa ya kusini.   Prof. Mkumbo aliwatoa hofu wananchi waliokuwa wakisubiri kufufuliwa kwa kiwanda kilichopoteza zaidi ya ajira 400, kuwa kupitia uongozi wa Rais, Samia Suluhu Hassan, wanaenda kuboresha na kutumia eneo hilo vizuri, kwa kuweka mtaa mkubwa wa viwanda utakaochochea maendeleo makubwa ya uchumi kwa wananchi wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.   Leonard Mgoyo, msimamizi wa Kiwanda kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa  (NDC), alisema wafanyakazi wa kiwanda hicho waliachishwa kazi Agosti 2009, lakini tangu mwaka 1998, kiwanda hakijawahi kufanya uzalishaji kufikia angalau asilimia 50 ya uwezo wake.   “Japo uwezo upo ila tatizo ni mabadiliko ya teknolojia na mitambo kuwa ya kizamani pia kilichozalishwa hakikuhitajika kabisa sokoni,” alisisitiza.   Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo, akizungumza baada ya Waziri Kitila kuzungumzia hilo alisema: “Arusha kuna matatizo makubwa ya ajira, tunaamini mkakati wa  kufufuka kwa eneo la  kiwanda hiki, kutatoa mwanga ili wananchi wa Arusha waweze kupata ajira na serikali iweze kupata kodi zitakazotokana na uzalishaji utakaokuwapo.”

Chanzo: ippmedia.com