Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Eneo la Umwagiliaji kuongezeka nchini hadi asilimia 89.9

Mndolwaaa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji nchini, Raymond Mndolwa

Tue, 30 Apr 2024 Chanzo: Mwananchi

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji nchini, Raymond Mndolwa amesema kukarabati na kujenga miradi mipya ya umwagiliaji nchini kutaongeza eneo la umwagiliaji na kufikia asilimia 81.9.

Mndolwa ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 30, 2024 wakati wa hafla ya kusaini mikataba ya miradi 20 ya umwagiliaji mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Mndolwa amesema kuwa tume ilipanga kujenga, kukarabati na kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika miradi 780 ndani ya kipindi cha miaka miwili.

"Miradi ya umwagiliaji huchukua zaidi ya miezi 18, hivyo kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika skimu hizo kwa miaka hii miwili kutaongeza eneo la umwagiliaji zaidi ya hekta 256,000 na kufanya eneo linalomwagiliwa kufikia hekta 983,465.46 sawa na asilimia 81.9 ya lengo la kufikisha hekta 1,200,000 ifikapo 2025 na ongezeko hilo litatengeneza ajira za kudumu takribani 1,352,127,” amesema Mndolwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema sekta ya kilimo inaendelea kufanya mageuzi ili kuongeza tija kwa Taifa na pato la wakulima wadogo.

"Sekta ya kilimo imeendelea kufanya mageuzi makubwa na kuwekeza katika maeneo ya msingi ili uongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara zaidi na kuongeza pato la wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha yao, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali ya awamu ya sita iliongeza bajeti ya sekta ya umwagiliaji kutoka Sh46.5 bilioni mwaka 2021/22 hadi Sh361.5 bilioni 2022/23 na mwaka 2023/2024 bajeti imeongezeka kufikia bilioni 373.5,”amesema Waziri Bashe.

Chanzo: Mwananchi