Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Elon Musk kuchukua malighafi Tanzania

Elon Musk Arejea Kwenye Nafasi Ya Mtu Tajiri Zaidi Duniani Bilionea Mmarekani Elon Musk.

Sun, 5 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati maombi yake ya leseni ya kutoa huduma za intaneti kupitia kampuni yake ya Starlink yakiwa yamewekewa kigingi na masharti ya serikali, Bilionea Mmarekani Elon Musk amepenya kwenye soko la Tanzania ambapo atanunua malighafi ya kutengenezea betri za magari ya umeme.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari wiki hii na wawakilishi wa kampuni hiyo, inasema kwamba kampuni ya Musk ya Tesla inayotengeneza magari ya umeme, imeingia mkataba wa kununua hadi tani 35,000 za malighafi aina ya Anode Active Material inayotumika kutengenezea betri za magari ya umeme kwa mwaka kutoka kampuni ya Magnis Energy Technologies Limited ya Australia kupitia kampuni yake tanzu ya Kitanzania ya Uranex Tanzania Limited.

"Tesla imekubali kununua kati ya tani 17,500 na 35,000 za Anode Active Material kwa mwaka kutoka Magnis Energy Technologies kuanzia mwezi Februari 2025 kwa kipindi cha miaka mitatu," inasema taarifa hiyo.

Tofauti na kuingiza fedha za kigeni, taarifa hiyo imesema makubaliano hayo yamekuja wakati mwafaka kwa sababu Tanzania kama nchi inategemea kunufaika zaidi na ajira pamoja na ujuzi kwa watu wake.

Uranex Tanzania Limited inamilikiwa na Magnis Energy Technologies Limited ya Australia na mradi wake wa uchimbaji wa madini ya kinywe (graphite) wa Nachu Graphite Project ulioko Ruangwa mkoani Lindi unajulikana duniani kwa kutoa bidhaa bora za madini hayo.

Tesla yenye makao yake jijini Austin, Marekani ni kampuni inayoongoza kwa utengenezaji wa magari ya umeme ambayo yanapigiwa chapuo na wanaharakati wa mazingira kama usafiri rafiki kwa mazingira kulinganisha na magari yanayotumia bidhaa za petroli yanayolaumiwa kwa kutoa hewa ukaa na kuongeza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika makubaliano hayo, Uranex Tanzania itasimamia mradi wa kinywe wa Nachu kuhakikisha inatoa bidhaa bora kwa ajili ya kusafirishwa kwenda kwa mteja ambaye ni Tesla.

Tangu mwaka jana, taarifa zilisambaa kwamba Bilionea Musk ambaye ni Mmarekani aliyezaliwa Afrika Kusini, aliwasilisha maombi nchini kupitia kampuni yake ya Starlink ya kuomba leseni ya kutoa huduma nafuu ya intaneti kupitia satelaiti.

Na hivi karibuni kulikuwa na sintofahamu kuhusu hatma ya maombi yake huku kukiwa na fununu kwenye mitandao ya kijamii kwamba aliwekewa mizengwe na kampuni za simu zinazotoa huduma za intaneti kwa Watanzania wengi kwa sasa.

Lakini Jumanne wiki hii, Nape Nnauye, Waziri wa Habari na Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, alilitolea ufafanuzi suala hilo, akisisitiza kwamba hakuna mizengwe bali kuna masharti ambayo mwomba leseni hajatekeleza.

“Kuna mambo mawili; kwanza tuliwaambia wafungue ofisi hapa Tanzania ili kukiwa na matatizo ya kimtandao, wateja wao waende hapo na si ofisini kwangu. Pili, tuliwaomba watuthibitishie namna watakavyotunza taarifa za wateja wao," alisema waziri huyo wakati wa ziara yake kwa vyombo vya habari vya IPP mkoani Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live