Bosi mpya wa Twitter na tajiri namba moja duniani, Elon Musk ametangaza msamaha wa jumla kwa akaunti zilizosimamishwa Twitter hatua iliyotafsiriwa kuwa "waeneza chuki" watarejea kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii.
Mmiliki huyo amesema msamaha kwa watumiaji waliozuiwa utaanza wiki ijayo baada ya kura nyingi kwenye akaunti yake kuunga mkono hatua hiyo.
Akaunti zilizosimamishwa kwenye Twitter ni pamoja na mshauri wa zamani wa Donald Trump, Steve Bannon, mchambuzi wa Uingereza Katie Hopkins na David Duke, mtaalamu wa mifumo wa zamani wa Ku Klux Klan.
Musk alikuwa ameanzisha kura ya maoni Jumatano akiuliza kama msamaha wa jumla unapaswa kutolewa kwa akaunti ambazo ‘hazikuvunja sheria’.
Musk hakutaja sheria alizomaanisha. Zaidi ya kura milioni 3.1 zilirekodiwa na asilimia 72 zikiunga mkono msamaha.