Katika hatua ambayo haikutarajiwa Elon Musk ameiomba mahakama ya California kufuta kesi ya kisheria dhidi ya OpenAI na mkuu wake Sam Altman, ambayo iliwashutumu kwa kutelekeza kazi ya kuanzisha kampuni hiyo ya kutengeneza akili mnemba (AI) kwa manufaa ya binadamu.
Nyaraka zilizowasilishwa na mawakili wa mabilionea huyo ziliomba kesi hiyo iliyodumu kwa miezi kadhaa itupiliwe mbali bila kutoa sababu yoyote ya kuhama.
Ziliwasilishwa siku moja tu kabla ya mahakama kutarajiwa kusikiliza ombi la msanidi programu wa ChatGPT kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali.
BBC imewasiliana na wakili wa Bw Musk na OpenAI kwa maoni.
Nyaraka za hivi punde kutoka kwa Musk ziliomba kesi hiyo itupiliwe mbali "bila upendeleo", ikimaanisha kuwa Bw Musk bado anaweza kuifungua tena baadaye.
Mkuu huyo wa kampuni ya Tesla alifungua kesi dhidi ya OpenAI mwishoni mwa Februari mwaka huu, akisema kampuni aliyoisaidia kufunguliwa mwaka 2015 ilikuwa imepotoka kwenye malengo yake ya kujitolea ikilenga kutafuta pesa.
OpenAI ilipinga kuwa Bw Musk hapo awali aliunga mkono wazo la muundo wa faida na hata kupendekeza kuunganishwa na kampuni yake ya magari ya umeme ya Tesla.
Ugomvi wa pande mbili ulizidi mapema wiki hii baada ya kampuni ya Apple kuzindua ushirikiano na OpenAI ili kuimarisha mifumo ya uendeshaji na chatbot ya OpenAI ya ChatGPT.
Baada ya tangazo hilo, Bw Musk alichapisha jumbe kadhaa kwenye mtandao wake wa kijamii wa X, ambao zamani ulijulikana kama Twitter, akikosoa uhusiano huo.