Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Elimu yaanza kuepusha mikopo umiza

Mkopo Elimu yaanza kuepusha mikopo umiza

Mon, 28 Jun 2021 Chanzo: ippmedia.com

Elimu hiyo imekuwa ikitolewa na Taasisi Isiyokuwa ya kiserikali ya Msaada wa Kisheria (LSF), yenye makao Makuu yake jijini Dar es Salaam na ina tawi katika eneo la Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (TEKU).

Maofisa wa Taasisi hiyo wamekuwa wakitoa elimu hiyo katika maeneo mbalimbali ya mikusanyiko ya watu ikiwamo kwenye vituo vya mabasi, vituo vya bodaboda na bajaji.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa utoaji wa elimu hiyo katika vituo vya mabasi vya Kabwe na Uyole, Meneja wa LSF, Aggripa Senka, alisema wananchi wengi wamejiingiza kwenye mikopo umiza bila kujua masharti ya mikopo hiyo.

Alisema kutokana na hali hiyo, wananchi hao wamekuwa wakijikuta katika wakati mgumu kutokana na wakopeshaji hao kuchukua mali zao zikiwamo nyumba, vyombo vya usafiri, mashamba pamoja na mali zingine kwa ajili ya kufidia mikopo hiyo.

“Mikopo hii imekuwa ya kilaghai, sana na wakati mwingine imekuwa ikisababisha migogoro kwenye familia, kutokana na baadhi ya wakopaji kutowashirikisha wenza wao, sasa sisi tunawaelimisha wananchi waiogope mikopo hii na badala yake wakakope kwenye taasisi zilizosajiliwa,”  alisema Senka.

Mkurugenzi wa LSF, Wakili Martha Gwalema, alisema katika kampeni hiyo wamefanikiwa kuwafikia wananchi wengi na kwamba katika maeneo yote waliyopita walikutana na wananchi ambao wameumizwa na mikopo hiyo.

Alisema baadhi ya wananchi waliochukua mikopo hiyo na mali zao kuchukuliwa walirejeshewa kwa ushirikiano kati ya Taasisi hiyo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), na kwamba kurejeshwa kwa mali hizo ni sehemu ya mafanikio ya taasisi hiyo.

“Katika maeneo tuliyopita tumebaini kuwa ni wananchi wengi wameumizwa na mikopo hii, mbali na kuwasaidia kurejeshewa mali zao pia tumewapatia elimu itakayowasaidia kuepuka mikopo hii,” alisema Martha.

Kwa upande wake, Wakili Ezelina Mahenge, ambaye ni miongoni mwa waelimishaji, aliwaasa wananchi kabla ya kuingia mikataba ya mikopo hiyo wanapaswa kusoma kwa makini masharti, na kwamba ikiwezekana kuwatumia wanasheria kuwatafsiria masharti hayo.

Alisema ni vema wakopaji kushirikiana na wenza wao ama watu wao wa karibu ili kuepusha migogoro katika ndoa sambamba na kuzuia upotevu wa mali walizozihangaikia kwa muda mrefu.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata elimu hiyo ambao wengi walikuwa wanawake, walisema wengi ndoa zao zimeyumba kutokana na mikopo hiyo.

Mmoja wa wanawake hao, Subira Mwalembe alisema riba za mikopo hiyo ni kubwa, na imekuwa ikiwaumiza kwa maelezo kuwa wakikopa Sh. 50,000 wamekuwa wakilipa mpaka Sh. 1,000,000.

Mpaka sasa Taasisi ya LSF imewafikia zaidi ya wananchi 220,000 katika kipindi kisichozidi miezi sita.

Chanzo: ippmedia.com