Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)) imetangaza kupungua kwa bei za rejareja za petroli, dizeli na mafuta ya taa.
Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Modestus Lumato kuhusu bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli kuanzia leo ilieleza bei hizo zitaanza kutumika kuanzia leo.
Lumato alieleza kuwa kwa Februari mwaka huu bei za rejareja za mafuta ya dizeli na mafuta ya taa yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimeshuka kwa shilingi 190 kwa lita na shilingi 142 kwa lita, mtawalia, ikilinganishwa na toleo la tarehe 4 Januari mwaka huu na bei ya rejareja ya mafuta ya petroli haibadiliki.
Alieleza kuwa kwa mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara), bei za rejareja mwezi huu kwa mafuta ya petroli na dizeli zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la Januari 4, mwaka huu. Lumato alieleza kuwa kwa mikoa ya Kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma), bei za rejareja za mwezi huu kwa mafuta ya petroli na dizeli zimeshuka kwa shilingi 118/lita na shilingi 160 kwa lita, mtawalia, ikilinganishwa na toleo la tarehe 4 Januari mwaka huu.