Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EWURA yasitisha bei mpya ya mafuta

Mafuta 2 EWURA yasitisha bei mpya ya mafuta

Thu, 2 Sep 2021 Chanzo: Mwananchi

Serikali imesitisha bei za mafuta zilizoanza kutumika leo kote nchini na kuunda timu ya kuchunguza na kuangalia viashiria vinavyofanya kupanda kwa bei.

Akizungumza katika viwanja vya Bunge leo, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Godfrey Chibulunje amesema kila Jumatano ya mwisho wa mwezi Ewura hutangaza viwango vipya vya bei ya mafuta nchini.

Amesema kwa kuwa bei hiyo imeonekana kupanda na itaendelea kupanda, hivyo Serikali imeamua kuchukua hatua ya kusitisha ili bei zilizokuwa zinatumika mwezi uliopita (Agosti) ziendelee kutumika.

Chibulunje amesema Serikali imeunda timu maalum ya kuchunguza na kuangalia viashiria gani vinafanya bei kuongezeka.

Amesema baada ya timu hiyo kufanya kazi watarudi tena kwa wananhi kutoa maelekezo maalum.

Amesema timu hiyo imehusisha Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Nishati na Madini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ewura na taasisi nyingine zinazoonekana kufanya kazi hiyo.

Hata hivyo, alisema timu hiyo haijapewa maelekezo ya muda itakayofanya kazi hiyo.

“Lengo ni kuashiria gani vimefanya kupanda bei kuna mambo mengi ambayo inawezekana kuna makusanyo walikuwa wanakusanya Serikali imeshatimiza malengo yake tutaangalia yote,”amesema

Amesema wataangalia kuwa ni mambo gani ambayo wameyatimiza na kupendekeza kutolewa.

Mafuta hayo yamepanda ikiwa ni miezi miwili tangu yalipopanda kwa mara ya mwisho Julai Mosi 2021 bei ambayo ilianza kulalamikiwa. Mwaka huu ni mara ya tatu kupanda bei za mafuta mara ya kwanza ilikuwa Aprili.

Meneja mawasiliano na uhusiano wa amlaka hiyo Titus Kaguo juzi alitaja viwango tofauti vilivyopanda kuwa ni katika bandari ya Dar es Salaam ambako petroli imepanda kwa Sh84, dizeli 29 wakati mafuta ya taa bei ikiongezeka kwa sh18.

"Bandari ya Tanga petroli imeongezeka kwa Sh53, dizeli 14 na mafuta ya taa yatabaki hivyo na bandari ya Mtwara Petrol imeongezeka Sh108 na dizeli Sh46," alisema Kaguo.

Kwa mujibu wa Meneja huyo, bei katika mikoa mingine itategemea na wanachukulia wapi mafuta hayo kati ya bandari hizo lakini bei ni elekezi.

Hata hivyo, alionya kwa baadhi ya wafanyabiashara kutotumia nafasi hiyo kupandisha bei zaidi ya iliyotangazwa na mamlaka kwani kufanya hivyo ni kosa.

Ametoa mfano wa baadhi ya maeneo petroli itauzwa itakavyouzwa ni Dar es Salaam Sh 2511 wakati wilaya ya Ngorongoro itazwa kwa Sh2680.

Chanzo: Mwananchi