Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ETS kutumika kudhibiti bidhaa bandia sokoni

Tue, 3 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katika mkakati wa kukabiliana na bidhaa feki sokoni, Serikali imeanzisha awamu ya pili ya utozaji kodi kupitia stempu za kielektroniki (ETS) ambayo itaainisha uwepo wa bidhaa feki na zisizo feki.

Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo alisema matumizi ya ETS ni vita ya kudhibiti bidhaa feki na kuzinduliwa kwa awamu yake ya pili ni mwendelezo wa vita hiyo.

Akizungumza baada ya mkutano wa kifungua kinywa (staftahi) ulioandaliwa na Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam juzi, Kayombo alisema mpango uliopo sasa ni kuja na mfumo ambao mteja ataona kwa undani bidhaa anayoinunua kupitia simu ya mkononi.

“Suala la bidhaa feki si tu kwamba ni changamoto kwa biashara, bali pia kwa Serikali kwa sababu tunapoteza mamilioni ya kodi na matokeo yake tunashindwa kutekeleza miradi ya maendeleo,” alisema Kayombo.

Katika mkutano huo, wenye viwanda walilalamikia kuwepo kwa bidhaa feki sokoni wakisema kunazorotesha ushindani, jambo linalotakiwa kuchukuliwa hatua za haraka.

Akizungumzia suala hilo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema vita hiyo inapaswa kupiganwa na wadau wengi ikiwamo CTI inayotakiwa kuwataja wenzao wanaosababisha tatizo hilo.

Pia Soma

Advertisement   ?
Agosti Mosi mwaka huu, TRA ilitangaza kuanza kutumika kwa awamu ya pili ya stempu za kielekroniki kwa kampuni zinazozalisha vinywaji vya kaboni na vinywaji baridi.

Uamuzi wa matumizi ya stempu hizo yamehitimisha matumzi ya stempu za kawaida katika vita ya kupinga ukwepaji wa kodi na bidhaa feki.

Awamu ya kwanza ya stempu hizo katika mvinyo, pombe kali na sigara ilianza Januari mwaka huu.

Mfumo huo ulianza kufanya kazi kwa ujumla katika vinywaji vyenye kilevi, sigara na maji ya chupa kuanzia Juni 15, mwaka huu.

Mfumo huo unabadilisha matumizi ya stempu za karatasi zilizokuwa zikiwekwa kwenye sigara, mvinyo na pombe kali. Mfumo huo wa zamani uliwalenga waliokuwa wakidanganya katika ulipaji wa kodi na makosa yanayofanana na hayo.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa tangu ETS zilipoanza kutumika katika awamu ya kwanza kwenye tumbaku na vinywaji vyenye kilevi Januari mwaka huu, makusanyo ya ushuru wa forodha yameongeza kwa asilimia 22.7.

Kayombo alisema matumizi hayo katika vinywaji vya kaboni na baridi, yameiwezesha TRA kujua idadi ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kutakiwa kukatwa kodi.

Mbali na hiyo, alisema ETS zimeongeza mapato, wigo wa kodi na kuondoa ukwepaji wa kodi miongoni mwa wazalishaji.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz