Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ETS, EFD kutumika kuwadhibiti wakwepa kodi Mwaka wa fedha 2020/2021 - Serikali

98683 Pic+mapato ETS, EFD kutumika kuwadhibiti wakwepa kodi Mwaka wa fedha 2020/2021 - Serikali

Wed, 11 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ukusanyaji wa mapato ya kodi,  Serikali imesema itaendelea kuhimiza matumizi ya Stempu za kielektroniki (ETS), ili kuwadhibiti wale wanaokwepa kulipa kodi.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Machi 11, 2020 Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango alipokuwa awasilisha mapendekezo ya Serikali ya mpango wa maendeleo wa Taifa na ya kiwango na ukomo wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Waziri huyo amesema lengo la kufanya hivyo ni kutaka kuendelea kusimamia matumizi ya stempu hizo katika bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa na kupitia nyaraka za walipakodi.

Amesema tangu kuanza kwa matumizi yake, kupitia kwa nyaraka za walipakodi, lengo la kufanya usuluhishi wa kodi walizolipa kwa kujikadiria wao wenyewe linatekelezeka  kwa kulinganisha kiasi halisi walichopaswa kulipa kwa mujibu wa Sheria.

Pia amesema inachukua hatua mbalimbali ili kuongeza makusanyo zaidi.

Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuendelea kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za kodi na kuhakikisha mfumo wa usimamizi wa mashine za kielektroniki za kutolea risiti unatumika ipasavyo.

Pia Soma

Advertisement
Pia, amesema “tutaendelea na utoaji wa elimu kwa mlipakodi na dhana ya ‘ukinunua dai risiti na ukiuza toa risiti.’”

Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/20, iliyoidhinishiwa ina jumla ya Sh33.11 trilioni 33.11, ikijumuisha Sh20.86 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh12.25 trilioni 12.25 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. 

Waziri Mpango anasema jumla ya mapato ya ndani yalitarajiwa kuwa Sh23.05 trilioni na kati ya mapato hayo, Serikali ililenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh19.10 trilioni, mapato yasiyo ya kodi ya jumla ya Sh3.18 trilioni na mapato kutoka vyanzo vya Halmashauri ni Sh765.5 bilioni. Katika kipindi cha Julai 2019 hadi Januari 2020, mapato ya ndani yalifikia Sh11.87 trilioni sawa na asilimia 92.3 ya lengo la kukusanya Sh12 trilioni katika kipindi hicho. Amesema kati ya makusanyo hayo, mapato yanayokusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), yalikuwa Sh10.62 trilioni sawa na asilimia 96.9 ya makadirio ya Sh10.96 trilioni katika kipindi hicho. 

Waziri Mpango amesema katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Januari 2020, ufanisi wa kukusanya mapato ya kodi umeimarika na kufikia asilimia 96.9 ya lengo ikilinganishwa na ufanisi wa asilimia 88.6 katika kipindi cha Julai 2018 hadi Januari 2019, sawa na ukuaji wa asilimia 16.6.

Amesema sababu za ongezeko la mapato yaliyokusanywa na TRA ni pamoja na kuongezeka kwa utoaji wa elimu ya mlipakodi; wananchi kuhamasika kulipa kodi kutokana na kuimarika kwa utoaji wa huduma za kiuchumi na kijamii ikijumuisha maji, elimu, afya, miundombinu wezeshi ya barabara na umeme.

“Sababu nyingine ni kuendelea kuongezeka kwa uwazi katika usimamizi wa sheria za kodi,  uboreshaji wa huduma kwa mlipakodi, usimamizi wa matumizi ya mashine za kutolea risiti za kielektroniki hususan kwenye sekta ya usafirishaji wa bidhaa mbalimbali, kuendelea kuziba mianya ya ukwepaji kodi kwa kuwashirikisha kikamilifu na kuwaelimisha ipasavyo wale wote ambao wamekuwa wakibainika kukwepa kodi,” amesema waziri huyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz