Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EPZA inavyosaidia wakulima soko la malighafi

EPZA EPZA inavyosaidia wakulima soko la malighafi

Mon, 13 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAMLAKA ya Ukanda Maalum ya Uwekezaji na Mauzo Nje ya Nchi (EPZA), imesaidia kuwaunganisha wakulima kuuza malighafi katika viwanda na kuwahakikishia soko la uhakika na ongezeko la kipato kutoka kwenye mazao yao.

Meneja wa EPZA, Grace Lemunge, alipokuwa anaongea kuhusu ushiriki wao katika maonyesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere katika Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.

“Tumepiga hatua kubwa sana katika kuwapa wakulima taarifa muhimu pamoja na kuwaunganisha na wenye viwanda ambavyo vipo chini ya EPZA na hili limewasaidia sana katika kupata masoko ya uhakika na ongezeko la kipato,” alisema.

Alisema washiriki na wageni waliotembelea maonyesho ya mwaka huu, wana kwenda kwa wingi katika banda lao Sabasaba ili kupata maelezo ya kunufaika na motisha unaotolewa na mamlaka ya EPZA.

Lemunge alisema maonyesho hayo ni fursa muhimu ya kuwahabarisha wananchi na wakulima na wajasiriamali ili kuwaunganisha na masoko hasa viwanda ambavyo hutumia malighali ya kilimo.

EPZA imetumia maonyesho ya mwaka huu kuwaunganisha wakulima wa maparachichi na kiwanda kipya kilichopo mkoani Arusha kinachofanya kazi chini ya mwamvuli wa EPZA na kuwaongezea fursa kubwa ya soko la uhakika na kipato.

Mamlaka imekuwa ikifanya kazi kwa karibu sana na viwanda vinavyoongeza thamani mazao kama vile dengu, choroko na mbaazi ambavyo huuzwa katika masoko ya India na ya Asia.

Pia, EPZA imefanya kazi kwa karibu na wakulima wa ufuta na kuwaunganisha na wanunuzi ambao huuza katika masoko ya Asia na Ulaya.

Meneja Uhamasishaji Uwekezaji alisema katika maonyesho ya mwaka huu viwanda 16 vilivyo chini ya mwamvuli wa EPZA vimeshiriki na kuwahabarisha washiriki na wageni waliotembelea maonyesho hayo.

Baadhi ya viwanda hivyo ni DZ Cards ambacho kinashughulika na utengenezaji wa kadi za kieletroniki ili kurahisisha kufanya ununuzi wa bidhaa.

Kiwanda kingine ni Tooku Garments Co., Limited kinachozalisha nguo kwa ajili ya kuuza katika soko la Marekani.

Viwanda hivi vimekuwa chachu kubwa kutoa ajira kwa Watanzania wengi pamoja na kuchangia pato la taifa kupitia kodi mbalimbali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live