Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

EFTA yawekeza kuinua sekta ya kilimo nchini

WAKULIMA EFTA yawekeza kuinua sekta ya kilimo nchini

Mon, 22 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

TAASISI ya Usawa kwa Watanzania (Equity for Tanzania Limited-EFTA), imesema kuwa uwekezaji wa fedha na elimu kwenye sekta ya kilimo hasa kwa wakulima wadogo nchini kunaweza kuwa utatuzi wa changamoto ya sekta hiyo nchini.

Akizungumza na Nipashe, Meneja wa Masoko na Maendeleo ya Biashara wa EFTA, Peter Temu, alisema EFTA imetambua changamoto katika sekta ya kilimo nchini na hasa ukuaji wa uchumi na hivyo kuamua kuanzisha taasisi hiyo ili kusaidia wakulima wadogo wadogo.

Temu alisema kuwa kilimo kina mchango mkubwa kwa uchumi wa Tanzania na kuwa sekta hiyo imeonekana kuwa na changamoto kwa baadhi ya taasisi za mikopo na fedha.

Alisema kuwa EFTA Ltd ni mojawapo ya taasisi za kifedha zilizowekeza kiasi kikubwa sana kwenye kilimo na uchakataji mazao hapa nchini kwa kuelewa kuwa uchumi wa nchi yetu unategemea sana kilimo.

Alifafanua kuwa kilimo kwa Tanzania kinazalisha asilimia 90 ya chakula kinachohitajika ambapo asilimia 80 ya uzalishaji huo unatoka kwa wakulima wadogo wanaoishi vijijini na ambao teknolojia bado sio rafiki kwao au hawana kabisa zaidi ya kutegemea mvua na jembe la mkono.

"Hivyo tuliamua kuanzisha Taasisi hii kusaidia wakulima ikizingatiwa kuwa kilimo kinasaidia ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Tumewekeza zaidi ya Sh. bilioni 25 kwa kuwakopesha bila dhamana wakulima mashine mbalimbali za kilimo , matrekta na mashine zingine za kisasa ili kuondokana na changamoto ya kutumia jembe," alisema Temu.

Alisema pia EFTA imewekeza zaidi ya sh. bilioni tano katika kusaidia kuchakata mazao kwa wakulima wadogo na kuwafanya kubadili maisha yao kiuchumi.

Aliongeza kuwa kupitia EFTA wakulima wamebadili mfumo wao wa kilimo kwa kuzalisha kisasa zaidi na kwa wingi kwa kutumia matrekta na mashine zingine za kisasa zinazowafanya waondokane na kilimo cha zamani na kulima kisasa zaidi.

Temu alisema kuwa maisha ya wakulima wengi kupitia EFTA yamekuwa kiuchumi, mfano wameongeza mitaji, kusomesha watoto, kupanua biashara na kuongeza ajira kwa Watanzania,kuongeza uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa za ndani na pia kuunga mkono dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

Hata hivyo ,Temu alisema EFTA imekuwa suluhu kwa wakulima wengi kwa sababu haitozi dhamani ya kitu ikilinganishwa na taasisi zingine za mikopo na fedha ambazo changamoto kwa baadhi ya taasisi hizo ni kutoza ongezeko la thamani (VAT) wakati wa huduma na ukodishaji wa vifaa.

Aliongeza kuwa kwa sasa EFTA umeanza kutoa mikopo katika sekta ya usafirishaji ikihusisha mabasi makubwa ya mikoani, daladala, malori makubwa na magari aina zote ya kufanyia kazi, pia sekta ya utalii tunakopesha magari ya aina mbalimbali kwa ajili ya kuwasafirisha na kuwahudumia watalii kama njia ya kuinua uchumi wa nchi kupitia utalii.

"EFTA tumepita hatua zaidi kwani kwa sasa tumesaidia kwenye sekta ya ujenzi na pia walengwa wanaweza kupata magreda, makatapila na vifaa vya aina yoyote vinavyotumika katika ujezi wa aina yoyote ile. Pia tuna mashine mbalimbali na magari yaliyotumika tunayoyakopesha kwa bei nafuu ili tu kusaidia Watanzania", alisema Temu.

EFTA Ltd ni kampuni ilianzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kuwasaidia wajasiriamali na wakulima ambao walionekana kutokuweza kukopesheka na benki pamoja na taasisi zingine za kifedha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live