Mbunge wa Nkasi Kaskazini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)Aida Khenani, amesema mashine za risiti za kielektroniki (EFD Machine) kwa ajili ukusanyaji wa mapato hazimsaidii mfanyabiashara mdogo na kwa kuwa zinaisaidia serikali kwenye ukusanyaji wa kodi zitolewe bure.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Mei 6, 2022, Bungeni jijini Dodoma, wakati wa kuchangia hoja kwenye hati za Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara zilizowasilishwa Bungeni na Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Ashatu Kijaji.
"Ukiangalia utaratibu wa bei ya mashine ya EFD haumsaidii mfanyabiashara mdogo na kama mashine hii inaisaidia serikali kukusanya mapato ni kwanini serikali isitoe mashine hizi bure kwa wafanyabishara, na umuhimu wa mashine hii unaonekana pale mfanyabiashara mkubwa ana uhakika wa kufanya biashara zake na mdogo anaangalia mtaji wake wa laki 6 halafu mashine ni laki 8 nani anaweza kufanya hiyo biashara,"amesema Mbunge Khenani