Tanzania ni miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zilizofaidika na teknolojia ya akili bandia katika kutambua magonjwa ya zao la muhogo kwa kuangalia dalili zinazoonekana katika majani.
Katika mazungumzo na HabariLEO Afrika Mashariki jana, Mtafiti kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kilimo cha Kitropiki (IITA), Neema Mbilinyi, alizitaja nchi nyingine za EAC zinazonufaika na teknolojia hiyo kuwa ni Kenya, Uganda na Rwanda.
Kwa Tanzania, Mbilinyi alisema teknolojia hiyo inatumika zaidi katika mikoa ya Geita, Mwanza na Kasulu mkoani Kigoma na Mkuranga katika Mkoa wa Pwani.
Mkuu wa Idara ya Uchechemuzi na Uratibu wa Rasilimali wa IITA, Dk Regina Kapinga alisema kituo hicho kinashiriki kongamano hilo kwa njia mbalimbali ikiwamo maonesho ya utafiti wa mazao kama muhogo na ndizi. - Awali katika mazungumzo hayo kwenye maonesho ya mazao yaliyofanyika katika viwanja vya IITA ikiwa ni sehemu ya programu za kongamano kubwa la chakula linaloanza leo Dar es Salaam, Mbilinyi alizitaja nchi nyingine nje ya EAC kuwa ni Mexico na Brazil. - Alisema teknolojia hiyo inayotumia simu ya mkononi ya akili bandia iitwayo Nuru, ina uwezo wa kutatua changamoto zinazotokana na magonjwa yanayoathiri mazao na kutoa elimu juu ya utambuzi na udhibiti wake. - “Nuru ni akili bandia katika utambuzi wa magonjwa na wadudu wanaoshambulia mazao, ina uwezo wa kutambua uwepo wa magonjwa kwa kuangalia dalili zinazoonekana katika majani,” alisema Mbilinyi.