BARAZA la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) limesema makubaliano kuhusu Eneo la Biashara Huru Barani Afrika (AfCFTA) ni fursa kwa sekta binafsi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Mshauri wa Sera na Biashara kutoka EABC, Adrian Njau, aliliambia HabariLEO Afrika Mashariki mwanzoni mwa wiki kuwa nchi za EAC hazina budi kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika AfCFTA.
“AfCFTA ni fursa kwa sekta binafsi ya Afrika Mashariki. Ni vema sekta yetu ikachangamkia fursa zinazotokana na soko hili kubwa,” alisema Njau.
Alitoa ushauri huo wakati nchi za Umoja wa Afrika (AU) zikitarajia kukutana mjini Nairobi Kenya katika jukwaa mashuhuri la sekta binafsi linalofanyika leo na kesho.
“Watu katika nchi za EAC tusiwe watazamaji, bali tushiriki na tuhakikishe tunanufaika kupitia biashara na uwekezaji ndani ya eneo letu la Afrika Mashariki. “Aidha, sekta binafsi ijiweke tayari kwa ushindani na iwe tayari kukabiliana na changamoto zozote zitakazojitokeza katika utekelezaji wa AfCFTA,” aliongeza Njau.
Kwa mujibu wa Njau, matarajio ya nchi za EAC katika mkutano huo hususani wafanyabiashara na sekta binafsi kwa ujumla ni kupata ufahamu zaidi kuhusu AfCFTA.
Jukwaa hilo lina kaulimbiu isemayo: ‘Ushiriki wa Sekta Binafsi Katika Ukuaji Jumuishi na Maendeleo Endelevu Huku Ukiimarisha Biashara na Uwekezaji Kuelekea Utekelezaji wa AfCFTA.’ “Wafanyabiashara na sekta binafsi ya Afrika Mashariki kwa ujumla, watapata ufahamu na chachu zaidi ya kushiriki na kunufaika na utekelezaji wa makubaliano mbalimbali ya AfCFTA,” alisema Njau.
Aliongeza: “Cha msingi ni sekta zote kuanzia wafanyabiashara wadogo, wakati na wakubwa kushiriki katika utekelezaji wa AfCFTA na kuhakikisha kila kundi linanufaika na fursa za kibiashara na kiuchumi.”
Akizungumzia sekta ya utalii nchini, Njau alisema kwa maoni yake Bajeti ya Tanzania kwa Mwaka 2023/2024 iliyoondoa tozo kadhaa, itasaidia kuongeza kasi ya ukuaji uchumi.
“Hii ni jambo jema kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kwenye sekta ya utaili kwani imewaondolea mzigo hasa wale wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambao mapato yao ni chini ya shilingi milioni 200 kwa mwaka,” alisema.