Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dola ya Marekani yachachamaa sokoni, wadau watia neno

Dola Dola Juu Juu Dola ya Marekani yachachamaa sokoni, wadau watia neno

Fri, 30 Jun 2023 Chanzo: mwanachidigital

Uhaba wa Dola ya Marekani ni changamoto inayozikabili nchi mbalimbali duniani kwa sasa, kutokana na umuhimu wa sarafu hiyo inayotumika kwa kiasi kikubwa katika malipo ya biashara kimataifa.

Uhaba wa sarafu hiyo muhimu umesababisha hata viwango vyake vya kubadilishia fedha kuongezeka, hivi sasa dola imepanda thamani tangu mwanzoni mwa mwezi huu.

Kwa kulinganisha shilingi ya Tanzania nayo thamani yake dhidi ya dola imeendelea kupungua. Mei 31 dola moja ilikuwa ikibadilishwa kwa Sh2,365, lakini mpaka jana dola moja ilikuwa inabadilishwa kwa Sh2,430 sawa na ongezeko la Sh65 kwa kila dola moja.

Kuongezeka kwa viwango vya kubadilishia dola maana yake mtu anayehitaji dola atatakiwa kuwa na shilingi nyingi zaidi kuzipata kuliko ilivyokuwa mwezi mmoja uliopita.

Suala la upungufu na kuongezeka kwa viwango vya kubadilishia dola linakuwa nyeti kutokana na athari zake katika maendeleo ya uchumi ikizingatiwa kuwa nchi inaagiza bidhaa nyingi kutoka nje na dola ndiyo fedha inayotumika zaidi katika manunuzi.

Kwa kipindi cha mwaka ulioshia Aprili mwaka huu, Tanzania ilitumia dola bilioni 14.39 kwa ajili ya manunuzi nje ya nchi, kiasi ambacho ni sawa na wastani wa dola 1.19 bilioni kila mwezi. Kuongezeka au kupungua kwa dola dhidi ya shilingi kunakuwa na athari za moja kwa moja katika mnyororo wa usambazaji.

“Nilienda kununua dola benki wiki iliyopita wakaniambia hawatoi kwa watu ambao hawana akaunti kwenye benki hiyo, nilipoenda kwenye benki yangu nikaambiwa kiwango cha juu kutoa ni dola 1,000 na rate (kiwango cha kubadilisha) ilikuwa kubwa sana,” alisema Sarifa Tenda bila kutaja majina ya benki hizo.

Ufafanuzi wa BoT

Akizungumzia ongezeko hilo la bei ya dola dhidi ya shilingi, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba alisema si tatizo kwa Tanzania pekee, bali dunia nzima kwa kuwa kinachosababisha ni changamoto za kiulimwengu.

Tutuba alisema dola inachangia asilimia 83 ya thamani ya miamala yote inayofanywa kwa ajili ya biashara za kimataifa, ndiyo maana inakuwa na athari za moja kwa moja pindi inapoadiminika au kupanda sokoni.

Akieleza kwa nini dola inazidi kupanda dhidi ya sarafu nyingine, Tutuba anasema ni kuongezeka kwa uhitaji wake sokoni kwa kuwa sarafu ni bidhaa kama zilivyo bidhaa nyingine.

“Baada ya mlipuko wa Uviko-19 watu wengi waliathirika kiuchumi kiasi cha kula akiba zao, sasa kila mtu anafanya kazi kwa nguvu zaidi ili kuziba ombwe lililotokea wakati huo, viwanda vikifanya kazi sana na uhitaji wa malighafi, ambazo baadhi zinanunuliwa kwa dola, unaongezeka,” alisema.

Sababu nyingine alitaja ni vita vya Russia na Ukraine vilivyosababisha kupanda bei kwa baadhi ya bidhaa zinazohitajika duniani kama ngano na mafuta, hivyo wengi walitumia fedha nyingi zaidi (dola) kupata bidhaa hizo na nyinginezo.

Kadhalika, mabadiliko ya tabianchi yaliathiri mavuno na kuleta madhara ya kimiundombinu, na vyote vililazimisha watu kufanya manunuzi ya nje. Pia, alisema sera ya Marekani ya kudhibiti mfumuko wa bei iliyovuta sarafu nyingi za nchi hiyo kurudi nyumbani.

Anasema miongoni mwa hatua ni BoT kuendelea kuingiza dola kwenye mzunguko (wastani wa dola milioni 2 kila siku), kuhamasisha uzalishaji wa ndani ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi, ambazo huchukua fedha nyingi za kigeni.

Hatua nyingine iliyotajwa na Gavana ni ile iliyotangazwa hivi karibu ya Serikali kuanza kununua dhahabu na kuongeze tozo ya baadhi ya bidhaa zinazotoka nje ya nchi ili kupunguza kiasi kinachotakiwa kufanya manunuzi ya nje.

Na nyingine ni ile ya hivi karibuni ya kukumbusha umma kupunguza kutumia dola kwa manunuzi ambayo yanaweza kufanywa kwa sarafu ya ndani. “Katika hili tuliziagiza hata taasisi za Serikali kuacha kutoa ankara za kodi kwa raia,” alisema.

Juni 22 mwaka huu Serikali kwa mara ya tatu ilitoa katazo la matumizi ya fedha za kigeni ndani ya nchi, hatua iliyotafsiriwa na wachumi kuwa inalenga kushughulikia changamoto ya uhaba wa dola.

Kabla ya katazo hilo, chombo hicho cha juu cha usimamizi wa fedha kilitoa taarifa kama hiyo Agosti 2007 na nyingine Desemba 2017, msisitizo ukiwa ni uzingatiaji wa Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006.

“Katika siku za karibuni, imebainika kuwepo ukiukwaji wa tamko hilo. Hivyo, Benki Kuu inapenda kuukumbusha umma kwamba maagizo yaliyotolewa hapo awali kuhusu matumizi ya fedha za kigeni yanapaswa kuendelea kuzingatiwa,” ilieleza taarifa hiyo ya BoT.

Maoni ya wadau

Mwenendo wa bei na upatikanaji wa dola umemgusa Dk Tobias Swai, mhadhiri mwandamizi wa Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS) akisema dola ikipanda bei vitu vyote ambavyo nchi inategemea kutoka nje vinapanda, hivyo kama mwenendo utaendelea hivyo ni dhahiri kutakuwa na mfumuko wa bei.

“Mfano kama leo dola moja itakuwa Sh2,300 kesho iwe Sh2,400, mtu aliyeagiza malighafi zake nje ya nchi kwa kutumia dola, akizalisha bidhaa zake atataka auze kwa bei ambayo inamwezesha kununua malighafi hizohizo kwa bei iliyoko sokoni,” anasema Dk Swai.

Anasema hilo linaleta changamoto kubwa kwenye gharama za maisha kwa kuwa kuna bidhaa nyingi muhimu ambazo zinaingizwa kutoka nje na athari yake inakuwa haiishi mara moja.

“Leo dola ikipanda bei ya mafuta inapanda na bidhaa hiyo ikiwa juu inaathiri hadi bidhaa za ndani kwa kuwa ni muhimu kwa shughuli za usafirishaji,” anasema Swai. Anasema baada ya vita vya Russia na Ukraine watu walianza kufanya kampeni ya kuiweka kando dola, pengine hilo limeifanya Marekani kutaka kuuonyesha ulimwengu umuhimu wa sarafu hiyo.

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la wenye viwanda nchini (CTI), Hussein Sufian anasema athari za kupanda kwa dola bado hazijaonekana sokoni, lakini hali hiyo ikiendelea walaji wataathirika na uchumi kwa ujumla utayumba.

“Dola ikiongezeka kunakuwa na ongezeko la gharama za malighafi, hilo ndiyo kubwa zaidi kwa upande wetu wazalishaji, lakini dola huathiri kila kitu, husuani mnyororo wa usambazaji kwa kuwa hata mafuta yanaangizwa nje ya nchi,” anasema Sufian.

Anasema “bado sokoni athari za kupanda huku kwa dola hakujaonekana kwa kuwa watu bado wana mzigo wa zamani, kadiri siku zinavyozidi kwetu athari zake zitaanza kuonekana.”

Hata hivyo, Sufian alisema huenda athari zisiwe kubwa sana kwa kuwa baadhi ya bidhaa bei yake katika soko la dunia zilikwishaanza kushuka, akitolea mfano mafuta na ngano.

Sifa za Dola Dola ndiyo sarafu inayoaminiwa zaidi kuliko nyingine na miongoni mwa sifa zake kubwa ni kutumika kama sarafu ya miamala ya biashara za kimataifa na hifadhi ya ukwasi. Katika benki kuu zote duniani dola zilizohifadhiwa ni asilimia zaidi ya 60 ya fedha zote za kigeni.

Miongoni mwa changamoto zilizopo katika mataifa mengi zinatokana na pale dola inapoimarika dhidi ya sarafu nyingine, inakuwa vigumu kwa mataifa husika kulipa madeni yake ya nje, mengi yakiwa walikopwa kwa dola.

Athari za dola si kwa nchi tu, bali hata kampuni binafsi ambazo zina mikopo ya namna hiyo huimarika na uhaba wa dola umesababisha mawimbi ya mshtuko katika masoko ya fedha za kigeni na kusababisha kuongezeka kwa mfumuko wa bei na viwango vya riba.

Vilevile kuimarika na au uhaba wa dola husababisha mawimbi na mshtuko katika masoko ya kimataifa ya fedha za kigeni na kusababisha kuongezeka kwa mfumuko wa bei na viwango vya riba.

Historia ya dola

Mwaka 1944 wakati Vita vya Pili vya Dunia vikiendelea Dola ya Marekani kwa mara ya kwanza ilitambuliwa rasmi kama sarafu iliyotunzwa na nchi nyingi kama akiba ya fedha za kigeni, kuanzia hapo imetawala biashara za kimataifa na shughuli za kifedha.

Mpaka Desemba, 2022 jumla ya dola za Marekani zilikuwa ni asilimia 58.9 ya fedha zote za kigeni zilizohifadhiwa katika benki kuu za nchi mbalimbali, mataifa yenye nguvu kubwa ya kiuchumi yakiongoza kuwa na kiwango kikubwa.

Euro inashika nafasi ya pili kama sarafu iliyohifadhiwa zaidi katika nchi mbalimbali kwa asilimia 20.47, ya tatu ni Paundi ya Uingereza asilimia 5.51, Yen ya Japan asilimia 4.59, Yuani ya China asilimia 2.69 na dola ya Canada kwa asilimia 2.36.

Hadi mwishoni mwa 2022 jumla ya fedha za kigeni zilizokuwa zimehifadhiwa katika benki kuu zote zilikuwa na thamani ya Dola za Marekani 11.96 trilioni, kati ya hizo dola za Marekani ni 6.47 trilioni, euro 2.27 trilioni zilizobakia ni chini ya trilioni moja.

Takwimu za IMF zinaonyesha kuwa mwaka 1999 Dola ya Marekani ilikuwa asilimia 71 ya fedha zote za kigeni zilizowekwa kama akiba.

Chanzo: mwanachidigital