Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amewataka wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma kuchangamkia fursa zinazojitokeza kwa kujenga miundombinu wezeshi kwa wawekezaji na wageni kwani baada ya Serikali kuhamia jijini Dodoma kumekuwa na ongezeko la wageni kutoka sehemu mbalimbali Duniani.
Waziri Kijaji ameyasema hayo wakati wa Kikao kazi na wafanyabiashara wa Jiji la Dodoma ambapo kimewahusisha wajasiriamali na wafanyabiashara pamoja na majukwaa yanayojihusisha na ujasiriamali.
Amesema uchumi imara wa Taifa upo mikononi wa sekta binafsi hivyo amewahimiza wafanyabiashara hao kutumia fursa zote zinazojitokeza iwe ni sekta binafsi au kutoka serikalini ili kuendelea kukuza uchumi wa nchi.
Waziri Kijaji amewahimiza wajasiriamali kuwa waaminifu na Fedha zinazotolewa na Serikali kama sehemu ya mtaji ili kuwawezesha na wengine kupata hiyo fursa.
“Lazima tukubaliane na utaratibu uliowekwa uadilifu wetu, uaminifu wetu ni muhimu hakuna fedha za bure sehemu yeyote lazima uwe na uhakika wa fedha kurudi na mtu unae mpatia fedha hivyo tunatakiwa kumthibitishia Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama alivyo mtetezi wetu namba moja," amesema Dkt. Kijaji.
Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, amempongeza Waziri Kijaji kwa kukutana na kuzungumza na wafanyabiashara hao pamoja na kutatua changamoto na kero zilizokuwa kikwazo katika utekelezaji wa biashara zao.
"Mkoa wa Dodoma upo tayari kupokea wawekezaji na kuongeza idadi ya viwanda ili kuongeza na kukuza mapato ya Serikali na uchumi wa nchi ya Tanzania,” amesema Mhe. Senyamule.