Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Dk Felix Nandonde amesema kuanzishwa kwa kiwanda cha sukari Bagamoyo, Mkoa wa Pwani ni jambo kubwa ambalo litasaidia kupunguza uhaba wa sukari nchini.
Dk Nandonde amebainisha hayo leo Jumatano, Desemba 28, 2022 wakati akichangia mjadala kuhusu matukio ya mwaka 2022 katika Mwananchi Twitter Space.
Amesema matumizi ya sukari hapa nchini ni tani 450,000 lakini uzalishaji ni tani 378,400, hivyo kuna upungufu wa sukari wa karibu tani 100,000 ambazo zinaagizwa nje ya nchi ili kutosheleza mahitaji.
"Kwa sasa Bagamoyo Sugar wanazalisha tani 30,000 lakini kufikia mwaka 2030 watafikia tani 100,000. Wameanza vizuri kwenye hili na matumaini ni makubwa siku zijazo," amesema Dk Nandonde.
Jambo jingine alilogusia mwanazuoni huyo ni migogoro kati ya wafanyabiashara wadogo na serikali za mitaa ambazo zinawatimua katika maeneo wanayofanyia biashara.
"Serikali inatengeneza mazingira wezeshi na moja ya mambo ambayo wafanyabiashara wanahitaji ni maeneo ya kufanyia biashara. Hili linawezekana tukalipatia dawa," amesema Dk Nandonde.