Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mwinyi ataka mageuzi sekta ya kilimo

F40278d72f121865b3c64003de59e39b.PNG Dk Mwinyi ataka mageuzi sekta ya kilimo

Tue, 9 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameiagiza Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo itekeleze mageuzi katika sekta ya kilimo ili nchi ijitosheleze kwa chakula.

Dk Mwinyi alisema hayo jumatatu Dole, Kizimbani Wilaya ya Magharibi Unguja katika kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya wakulima, Nanenane.

Alisema dunia imeshuhudia uhaba wa chakula na kupanda kwa bei za vyakula kutokana na kuwepo kwa vita katika nchi zinazozalisha chakula.

Dk Mwinyi aliagiza wizara hiyo ije na mikakati kukabili tishio la uhaba wa chakula kwa kuongeza kasi ya ubunifu.

''Dunia kwa ujumla inashuhudia kwa sasa...vita vya Urusi na Ukraine tumeshuhudia uhaba wa chakula ikiwemo ngano na mafuta,'' alisema.

Dk Mwinyi alisema umefika wakati wa kuona vijana wanajikita katika kilimo kikiwemo cha mbogamboga ili wajiajiri.

Alisema mahitaji ya chakula ikiwemo mbogamboga ni makubwa huku akisema zipo baadhi ya hoteli zinaagiza mahitaji nje ya nchi.

''Tunataka kuona mahoteli yaliopo nchini hayaagizi tena mbogamboga nje ya nchi ambapo huu ni wakati wa kuwaingiza vijana katika kilimo cha aina hiyo ambacho kitatoa ajira moja kwa moja,'' alisema.

Kwa upande wa kilimo cha karafuu, Dk Mwinyi alisema wakati umefika Wizara ya Kilimo na Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) kushirikiana kuotesha mikarafuu mipya ichukue nafasi ya ile ya zamani.

Alisema bei ya karafuu katika soko la dunia bado ipo imara ambapo wakulima wanatakiwa kuongeza juhudi za kuotesha mikarafuu mipya ili kuongezeka kwa uzalishaji wa karafuu.

Mapema Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis alisema mikakati ya wizara hiyo ni kurudisha hadhi ya mazao ya viungo na chakula kwa ajili ya kuhakikisha Zanzibar inajitosheleza kwa chakula na kusafirisha ziada nje ya nchi.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Seif Shaaban Seif alisema maonesho ya Nanenane yameshirikisha wajasiriamali 155, taasisi na mashirika 52.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live