Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk. Mwinyi aitimua kampuni ya ujenzi Zanzibar

Mwinyi Pic Nnnn Dk. Mwinyi aitimua kampuni ya ujenzi Zanzibar

Mon, 18 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameifukuza Kampuni ya Ujenzi ya Associated Investment Service Ltd ya Dar es Salaam kufanya kazi Zanzibar kwa kile alichodai haina uwezo.

Pia, alisitisha mkataba wa mkandarasi huyo wa ujenzi wa Shule ya Mtopepo katika Shehia ya Monduli Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini.

Rais Mwinyi alichukua hatua hiyo jana, baada ya kutembelea ujenzi wa shule hiyo yenye ghorofa tatu.

Kwa mujibu wa mkataba huo ulioanza Februari mwaka huu, ujenzi unatakiwa kukamilika Agosti mwaka huu, lakini bado upo asilimia 35.

“Nimesikitishwa sana, kazi ya miezi sita na sasa inaelekea kwisha lakini hakuna kilichofanyika, huyu mkandarasi hafai, haya sio makubaliano yetu, nasitisha mkataba na aondoke asipewe kazi nyingine Zanzibar,” alisema Dk Mwinyi.

Mbali na mkandarasi huyo, pia Rais Mwinyi alionyesha kuchukizwa na mkandarasi mshauri Kampuni ya Edge Consultancy, akisema ameshindwa kutoa ushauri wake wa kitaalamu, hivyo na yeye hana uwezo kiutendaji. Advertisement

Pia, aliiagiza Wizara ya Elimu kuwa wakali na iwapo wakiendelea kuwakumbatia na kuwaonea muhali watu wasiokuwa na uwezo mambo yatazidi kuharibika.

Mradi wa ujenzi wa shule hiyo yenye vyumba 41, matundu ya vyoo 44, unagharimu Sh4.5 bilioni na ikikamilika itakuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 3,690, tayari mkandarasi alikuwa amelipwa Sh1.08 bilioni.

Mkandarasi wa mradi huo, Theodory Zani alisema eneo linapojengwa shule hiyo mazingira hayakuwa mazuri.

Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi amewataka viongozi na watendaji wa Serikali kuwa wabunifu na kutafuta njia mbadala kutatua kero zinazowakabili wananchi.

Rais Mwinyi alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti jana, wakati akikagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya elimu, afya na maji Wilaya ya Kaskazini Magharibi A Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Changamoto nyingi zipo ndani ya Serikali, viongozi wetu sio wabunifu kutatua changamoto za wananchi haraka, ukiangalia changamoto nyingi zipo ndani ya serikali, lazima tuwe wepesi,” alisema Rais Mwinyi.

Alisema Serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha huduma za jamii ambazo zimekosekana na kusababisha kero kwa muda mrefu zinatatulika na kupata majibu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live