Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mwinyi aishukuru Benki ya Dunia kuisaidia SMZ

Mwinyi Pc Data.png Dk Mwinyi aishukuru Benki ya Dunia kuisaidia SMZ

Wed, 13 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta za maendeleo.

Ametoa pongezi hizo jana Ikulu mjini Unguja alipozungumza na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Kusini mwa Afrika, Victoria Kwakwa.

Dk Mwinyi alisema Benki ya Dunia ina historia ya muda mrefu katika kuiunga mkono Zanzibar kwenye sekta za maendeleo na kwamba, Zanzibar ni miongoni mwa nchi zilizoathirika na Covid-19.

Alisema shughuli za utalii visiwani humo zimekuwa zikiimarika na akamweleza hatua zilizofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuendeleza miradi ya elimu na afya inayotokana na fedha za Covid-19 zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Aliishukuru na kuipongeza Benki ya Dunia kwa kuendelea kuisaidia Zanzibar katika miradi ya maendeleo na akaeleza vipaumbele vya SMZ katika kuimarisha miundombinu zikiwamo barabara, bandari na kuimarisha sekta ya uchumi wa buluu.

Alieleza namna sekta ya uchumi wa buluu ilivyochukua nafasi katika utalii, uvuvi, kuwasaidia akina mama wanaojishughulisha na kilimo cha mwani, bandari na nyinginezo.

Alimweleza hatua za SMZ kuhakikisha zao la mwani linapata thamani na wakulima wanafaidika na kilimo hicho.

Alimweleza namna serikali ilivyoweka kipaumbele na kutilia mkazo uimarishaji wa sekta ya elimu, maji, miundombinu ya barabara na huduma za kijamii.

Alimhakikishia Kwakwa kwamba SMZ itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na benki hiyo hasa kwa kutambua juhudi inazozichukua katika kuiunga mkono Zanzibar.

Kwakwa alimueleza Rais Dk Mwinyi namna Benki ya Dunia inavyofarajika na juhudi za SMZ kuendeleza na kuimarisha miradi ya maendeleo inayosimamiwa na benki hiyo.

Alimueleza hatua zinazochukuliwa kuhakikisha Zanzibar inafaidika kwa mara nyingine na fedha za utekelezaji miradi ya maendeleo kupitia dirisha jipya la Jumuiya ya Kimataifa ya Maendeleo (IDA 20).

Alimhakikishia kwamba Benki ya Dunia itaendelea kuunga mkono miradi ya maendeleo iliyopewa kipaumbele na SMZ ikiwamo miundombinu ya barabara na sekta nyingine.

Alisema Benki ya Dunia imekuwa na ushirikiano na Zanzibar katika nyanja za kijamii na kiuchumi ikiwamo ujenzi wa miundombinu, elimu, afya, mazingira na mengineyo mingi kupitia mikopo nafuu.

Alisema janga la Covid-19 limeathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi kwa nchi kadhaa zinazotegemea sekta ya utalii na kueleza matarajio yake kwamba Zanzibar itarudi katika hali yake ya mwanzo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live