Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mwinyi: Manunuzi yote yawe kidijitali

C2347bc0faffb7b06e79a57de5dfc661 Manunuzi yote yawe kidijitali

Sun, 26 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameziagiza wizara zote, mashirika, mikoa, wilaya, manispaa, mabaraza na halmashauri za miji kote nchini kuanza kutumia mfumo wa ununuzi kwa njia ya mtandao (eProcurement) kuanzia sasa.

Alitoa wito huo katika uzinduzi wa mfumo wa ununuzi kwa njia ya mtandao (eProcurement), hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar.

Alisema suala la manunuzi limegubikwa na urasimu na kuna nyakati shughuli za utekelezaji wa mipango serikalini huchelewa au kukwama kabisa kwenye vitengo vya manunuzi.

Alisema pamoja na vitengo vya manunuzi kutakiwa kuzingatia misingi ya uadilifu na uwazi lakini kumekuwepo na baadhi ya watumishi walioridhika na hali iliopo hivi sasa, hivyo kuibua urasimu, jambo linalowavunja moyo wazabuni, wawekezaji na wafanyabiashara wanaotoa huduma serikalini.

Aidha, alibainisha kuwepo baadhi ya viongozi na watendaji wanaojaribu kwa njia za siri kupinga matumizi ya mifumo ya kidijiti ili kulinda maslahi yao binafsi.

“Naagiza kila taasisi yenye jukumu la kufanya manunuzi ihakikishe inatumia mfumo huu katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 unaoanza,” alisema.

Aliagiza kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa watendaji wa ngazi zote watakaoharibu au kudharau kwa makusudi kutumia mfumo huo.

Dk Mwinyi alieleza kuwa juhudi za kuunda mifumo zinapaswa kuambatana na utekelezaji wa mikakati imara ya utoaji wa mafunzo kwa watendaji wanaosimamia mifumo hiyo, sambamba na elimu hiyo kutolewa kwa wananchi.

Alisema wazabuni na wafanyabiashara wanahitaji kupewa mafunzo ya msingi na kuelimishwa juu ya umuhimu wa kutumia mfumo huo mpya, sambamba na taasisi zinazosimamia utawala bora.

Alisema mfumo wa ununuzi kwa njia ya mtandao utaondoa urasimu, kuimarisha uwazi, uadilifu pamoja na kuondoa kasoro za uwajibikaji ambazo hutumika kupanua mianya ya rushwa.

Katika hatua nyingine, Dk Mwinyi alisema kumekuwepo changamoto katika mfumo wa matumizi ya mashine za risiti za kielektroniki (VFD), ikihusisha kuwepo wafanyabiashara wanaokataa kutumia mfumo huo kwa makusudi au kukosa elimu juu ya wajibu walionao katika kulipa kodi.

Alitumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi na watendaji kushirikiana na Bodi ya Mapato (ZRB) katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa njia ya utoaji risiti za kielektroniki.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman alisema mfumo huo utaleta mafanikio makubwa na kubainisha azma ya wizara hiyo kuhakikisha hauchezewi.

Aidha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Saada Mkuya Salum alisema utekelezaji wa mfumo huo hautakuwa jambo la hiari, hivyo akaahidi kuusimamia kikamilifu huku akibainisha kuwepo kwa uadilifu wa kiwango cha chini kwa sasa katika eneo la manunuzi serikalini.

Alisema Wizara hiyo inakamilisha taratibu za kubadili sheria ya manunuzi ya mwaka 2011 ili iweze kuendana na wakati uliopo na hivyo akatumia fursa hiyo kuwataka viongozi serikalini kuwa tayari kwa jambo hilo.

Mapema, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil alisema lengo la kuandaa mfumo huo ni kuongeza ufanisi na kuwepo usahihi katika mchakato wa manunuzi serikalini.

Alisema ushirikiano mzuri waliopata kutoka sekta mbalimbali umechangia kwa kiasi kikubwa kuandaa mfumo huo ambao ni bora katika nchi za Afrika Mashariki.

Alieleza utekelezaji wa mfumo huo utawezesha na kufanikisha dhamira ya serikali ya kupunguza gharama, muda wa zabuni, kuwepo uwazi na kuleta ufanisi katika zabuni, kutoa huduma bora za kifedha, sambamba na kupunguza wizi na mianya ya rushwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live