Dodoma. Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Dk Mwigulu Nchemba amesema ili kuweka mazingira rafiki ya kufanya biashara nchini, Serikali ipeleke muswada wa sheria bungeni wa kuziunganisha taasisi mbalimbali.
Waziri huyo wa zamani wa Mambo ya Ndani ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 15, 2019 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara mwaka 2019/2020 ya Sh100.38 bilioni ambayo iliwasilishwa jana Jumanne na inatarajiwa kuhitimishwa leo jioni.
“Tunatofautiana katika jambo hili la viwanda, wapo wanaoona hakuna kazi iliyofanyika na wapo tunaona yapo yaliyofanyika,” amesema Dk Mwigulu.
Amesema Serikali imeliona hilo na kuandaa mpango mkakati wa kuhakikisha mazingira ya kufanya biashara nchini yanakuwa mazuri ikiwamo kuandaa dira ya namna ya kutatua changamoto hizo.
“Kama ambavyo Serikali ilileta sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii, ilete sheria itakayoweka mazingira kuwa rafiki katika ufanyaji wa biashara. Tukiunganisha taasisi hizo, zile tozo zinazoleta matatizo kwa wananchi wetu zitakuwa zimefutika.”
“Tutakuwa tumetatua kero ya wananchi kusubiri muda mrefu na zikiunganishwa zitapunguza mlolongo,” amesema Dk Mwigulu
Pia Soma
- Askofu mstaafu Mmole afariki dunia, kuzikwa Mei 21
- Mwanafunzi mwingine ajali ya Babati afariki dunia
- Serikali ya Tanzania yataja sababu kukwama mafuta ya kula bandarini