Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mpango akanyaga Mtwara siku 57 tangu alipopigwa ‘stop’

13367 MPANGO+PIC TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ametua mkoani Mtwara zikiwa zimepita siku 57 tangu mbunge wa Tandahimba (CUF), Ahmad Katani alipotangaza bungeni ‘kumpiga stop’ kukanyaga mikoa ya Lindi na Mtwara.

Katani alisema hayo Juni 25, bungeni jijini Dodoma wakati akiitaka Serikali kutoa fedha za wakulima zilizotokana na ushuru wa asilimia 65 ya mauzo ya korosho ghafi nje ya nchi.

Mbunge huyo aliyetumia dakika tano kuchangia Bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19, alisema kama fedha hizo zaidi ya Sh200 bilioni hazitatolewa, Waziri Mpango asikanyage katika mikoa hiyo.

“Hizi fedha tusipozipata Dk Mpango usikanyage Lindi na Mtwara. Hata fedha zilizopo kisheria unazichukua,” alisema Katani.

“Wewe (Dk Mpango) ni waziri wa ajabu ambaye hujapata kutokea. CCM mnasema ni chama cha wanyonge hao wa aina gani? Wakulima wanaolima korosho kwa jembe la mkono mnachukua fedha zao, huna huruma.”

Katika mchango wake huo, Katani alisema, “Mnapotosha umma wa Watanzania, mmekuja bungeni kusimamia Watanzania lakini mnashangilia wanavyoonewa na kudhulumiwa. Hawa wabunge wanaotoka majimbo ya Ikulu ni shida sana.”

Akijibu hoja hiyo Juni 26 wakati akihitimisha mjadala wa Bajeti ya Serikali aliyoiwasilisha Juni 14, Dk Mpango alisema atakwenda Lindi na Mtwara na hakuna mtu wa kumzuia. Alisema iwapo kuna mwenye chuki binafsi anamwombea msamaha kwa Mungu.

“Kama yupo mtu ana chuki binafsi na Philip Mpango namwombea msamaha kwa Mwenyezi Mungu na niwatahadharishe wanaokula fedha za umma wanakula sumu,” alisema waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa.

“Mimi Philip Mpango siwezi kamwe kuwahujumu wakulima wa Mkoa wa Lindi na niwahakikishie Watanzania kwamba, Mtwara na Lindi nitakwenda iwe kutimiza wajibu wangu na ni uhuru wangu na hata ikibidi kufa katika kulitumikia Taifa.”

Katika kutekeleza hilo, juzi alianza ziara ya kikazi mkoani Mtwara ambako alikutana na wafanyabiashara kutoka mkoani humo. Pia alitembelea taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa wizara hiyo, Benny Mwaipaja imesema Dk Mpango alitembelea Kituo cha Forodha cha Kilambo kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.

Mwaipaja aliyezungumza na Mwananchi kuhusu ziara hiyo, alisema: “Hii ni ziara ya kwanza tangu Bunge lilipomalizika na alikuwa hajaenda Mtwara kipindi kirefu.”

Katika ziara hiyo, wakazi wa Kijiji cha Kilambo waliiomba Serikali iwasaidie kutafuta mwekezaji atakayejenga kiwanda cha kusindika matunda na mazao ya kilimo.

Walisema ombi hilo linatokana na kijiji hicho kuwa na matunda na mazao mengi yanayokosa soko.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mohamed Mkama alisema wanazo fursa nyingi za kilimo zinazohitaji viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na kutoa ajira kwa vijana.

Alisema kijiji chao kinapakana na nchi ya Msumbiji na kuna mwingiliano mkubwa wa watu kibiashara na uhusiano wa kijamii.

“Watu kutoka Msumbiji wananunua chakula na bidhaa nyingine kutoka kwetu, lakini tunawauzia bidhaa bila kuongeza thamani, hivyo uwepo wa kiwanda utakuza uchumi wa kijiji chetu. Tunakuomba waziri wa Fedha utusaidie kupata kiwanda ili nasi tuweze kunufaika,” alisema Mkama.

Akijibu ombi hilo, Dk Mpango alisema inabidi ufanyike utafiti wa kutosha ili kubaini wingi wa mazao yanayozalishwa na wakulima wa kijiji hicho na vijiji jirani kwa ajili ya kupata takwimu sahihi za uzalishaji.

“Tukiwa na uhakika huo hata mwekezaji anayekuja tutamwambia kwa mwaka mmoja, kwa wastani kijiji hiki na vijiji jirani vinazalisha maembe kiasi fulani. Kwa hiyo, wazo la kutaka kuwa na kiwanda ni zuri lakini linahitaji kufanyiwa kazi zaidi,” alisema waziri huyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz