Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Mpango aagiza wadau kutafuta suluhisho uhaba fedha za kigeni

Dkt Mpango Afungua Kikao Cha Kiufundi Cha Mawaziri Nchi Za Afrika Dk Mpango aagiza wadau kutafuta suluhisho uhaba fedha za kigeni

Fri, 8 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewaagiza wadau wa sekta ya fedha nchini Tanzania kutafakari kwa kina na kupatia ufumbuzi wa changamoto ya uhaba wa fedha za kigeni uliopo nchini.

Amesema usimamizi na udhibiti wa benki na taasisi za fedha ni msingi wa sekta iliyo imara na wataalamu wanapaswa kutoa kipaumbele katika eneo hilo, ili kuhakikisha utulivu na ustahimilivu katika sekta ya fedha hasa kipindi cha changamoto za kiuchumi.

Dk Mpango amesema hayo leo Alhamisi, Machi 7, 2024 jijini Arusha alipozungumza kwenye kongamano la 21 la taasisi za fedha linaloongozwa na mada kuu isemayo ‘Kuimarisha ustahimilivu wa sekta ya fedha nyakati za changamoto za kiuchumi.’

Amesema licha ya jitihada zilizofanyika za kuimarisha uwezo wa sekta ya fedha nchini, ili kuimarisha misukosuko, ni muhimu wadau hao wa fedha nchini kuja na mawazo ili kupunguza uhaba wa fedha za kigeni nchini.

“Ninawaomba pia washiriki kutafakari kwa kina changamoto ya uhaba wa fedha za kigeni iliyopo hivi sasa na hatua gani za muda mfupi na wa kati ambazo inabidi zichukuliwe zaidi ya hatua za urekebu zinazochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Yafaa kongamano hili lijadili nafasi ya kutumia viwango nyumbufu vya ubadilishanaji fedha katika kudhibiti uhaba wa fedha za kigeni,” amesema Dk Mpango.

Ameshukuru jitihada zilizofanyika za kuimarisha uwezo wa sekta ya fedha nchini, ili kuhimili misukosuko, akitaka kongamano hilo liwe kichocheo cha maboresho katika sekta ya fedha.

“Ni vema BoT na taasisi zote za fedha nchini zisibweteke, dhoruba za kiuchumi duniani bado zinavuma kwa nguvu na kuna maeneo ambayo bado yana changamoto, hivyo hatuna budi kupitia mara kwa mara sheria, kanuni na miongozo na usimamizi wa taasisi za fedha ili kubaini mapema maeneo yenye udhaifu,”ameongeza Dk Mpango.

Amesema idadi ya watu wanaotumia huduma rasmi za fedha nchini iliongezeka hadi kufikia asilimia 76 mwaka 2023, kutoka asilimia 65 mwaka 2017.

Amesema mikopo iliyotolewa na benki kwa sekta binafsi imeongezeka baada ya Uviko-19 akitolea mfano mwaka 2022/23, ukuaji wa mikopo ulifikia wastani wa asilimia 19.8 ikilinganishwa na asilimia 6.6 katika miaka miwili iliyotangulia.

“Upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu ni muhimu kwa ukuaji wa Uchumi, hata hivyo, gharama ya mikopo katika soko la Tanzania bado iko juu na siyo rafiki kwa ukuaji wa uchumi, muangalie gharama hizo hasa kwa wajasiriamali wadogo na wa kati,” amesema Dk Mpango.

Awali akizungumza katika kongamano hilo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema mkutano huo umekutanisha washiriki 1,000 ambao wanatarajia kujadiliana mada tatu ikiwemo ufanisi na uhimilivu wa taasisi za fedha wakati wa majanga.

Katika hatua nyingine, BoT imezindua Mfumo wa Taifa wa Malipo ya papo kwa papo (TIPS), ulioanza kwa majaribio Agosti 2022 na benki tatu na kampuni mbili za mawasiliano ya simu, ambapo sasa benki zote na kampuni za mawasiliano ya simu zimeunganishwa.

Amesema licha ya changamoto ya kiuchumi duniani, uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa wastani wa asilimia 4.8 katika kipindi cha mwaka 2020/22 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 2.3 wa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na kati ya mwaka 2020/23 mfumuko wa bei ulikuwa wa wastani wa asilimia 3.8 chini ya lengo la kati la nchi la asilimia tano.

Naye Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, amesema sekta ya fedha Tanzania imeonyesha uhimilivu katika kupambana na changamoto za uchumi wa dunia za hivi karibuni ambapo uimara wa sekta ya benki umesaidiwa na uwiano mzuri wa mtaji na ukwasi ambao ulikuwa juu ya mahitaji ya chini ya udhibiti.

“Mikopo hatarishi pia imebakia katika viwango vya chini kama inavyoonekana katika kupungua kwa mikopo chechefu ambayo ipo chini ya kikomo cha asilimia tano ya mikopo yote, sekta ya bima pia iliweza kuhimili changamoto kwa kuwa na mtaji wa ukwasi wa kutosha,” amesema.

Ameongeza kuwa matokeo ya utafiti wa FinScope wa mwaka 2023 umeonyesha upatikanaji wa huduma rasmi za kifedha nchini uliongezeka kutoka asilimia 86 mwaka 2017 hadi 89 mwaka 2023, matumizi ya huduma rasmi za kifedha yaliongezeka kutoka asilimia 65 hadi 76.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live