Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Kimei aondoka CRDB kabla ya muda wake

20621 Kimei+pic TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Miezi minane kabla ya kukamilika kwa mkataba wake, mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei ametangaza kuachia madaraka yake na kupisha damu mpya.

Disemba mwaka jana, Dk Kimei alitangaza nia yake ya kustaafu utumishi wa benki hiyo akiipa miezi 19 kumtafuta mrithi wake. Muda huo ulikuwa na ziada ya mwezi mmoja kwani utaratibu wa benki hiyo kujaza nafasi hiyo ya juu zaidi ni miezi 18.

Hata hivyo, siku tatu baada ya kutambulishwa na kupokelewa kwa mrithi wake, Abdulmajid Nsekela, mtaalamu huyo wa uchumi ametangaza kujiondoa kwenye majukumu ya kila siku.

“Amechukua (likizo ambayo ataendelea kulipwa kama mkurugenzi wa benki) gardening leave. Kwa akipindi chote kilichobaki ataendelea kutambulika kama mfanyakazi wa CRDB ila hatolazimika kuja ofisini kwa kazi za kila siku,” amesema Tully Mwambapa, mkurugenzi wa masoko na huduma kwa wateja wa benki hiyo.

Mwezi uliopita, bodi ya wakurugenzi wa CRDB ilimtangaza Nsekela kuwa mkurugenzi mtendaji mpya wa benki hiyo kuchukua nafasi ya Dk Kimei aliyeiongoza kwa zaidi ya miongo miwili na kuipa mafanikio mengi.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Ally Laay alisema Nsekela atakuwa anakabidhiwa ofisi mpaka Mei mwakani atakapostaafu Dk Kimei. Kinyume na matarajio hayo, leo, Oktoba 03 mchumi huyo mwandamizi ametangaza kuchukua likizo hivyo kujiondoa ofisini.

Hata hivyo, Tully amesema kwa miezi iliyobaki, Dk Kimei ataendelea kumpa Nsekela ushirikiano unaohitajika.

“Atakuwa anamsaidia kutoka nyumbani…itakumbukwa, Dk Kimei amemlea kitaaluma Nsekela miaka ya nyuma alipokuwa anafanyakazi na benki hii. Ataendelea kumsaidia kila atakapohitaji,” amesema mkurugenzi huyo wa uhusiano.

Nsekela ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 na wakati anateuliwa kuiongoza benki hiyo kubwa kwa amana zinazozidi Sh5 trilioni alikuwa mkurugenzi wa wateja wadogo wa benki ya NMB.

Katika miaka hiyo, 10 aliipata akiwa CRDB alikoanzia kazi mwaka 2007 kabla hajajiunga na NMB alikodumu kwa muongo mmoja mwingine.

Taarifa za mwanzo zilieleza makabidhiano ya ofisi yangefanyika kuanzia Januari Mosi mpaka Mei 31 na kumruhusu Dk Kimei kupumzika na kusimamia mambo yake binafsi kama yeye mwenyewe alivyosema kuwa ndio utakuwa mustakabali wake.

Soma zaidi:

Wadau wamzungumzia bosi mpya CRDB

Nsekela amrithi Dk Kimei CRDB

Chanzo: mwananchi.co.tz