Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Kijaji awang'ata sikio watumishi FCC

Dkt Kijaji Awataka Wafanyabiashara Dodoma Kuchangamkia Fursa Dk Kijaji awang'ata sikio watumishi FCC

Wed, 6 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), imetakiwa kusimamia sheria na kulilinda soko la bidhaa nchini, lisiharibiwe na wafanyabiashara wenye nia ovu ya kutaka kulihodhi.

Hayo yamesemwa leo Desemba 05, 2023 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji katika hafla ya kilele cha maadhimisho ya siku ya ushindani duniani, yaliyofanyika jijini hapa.

Amesema mamlaka hiyo isipokuwa makini soko la bidhaa nchini linaweza kuharibiwa kwa baadhi ya watu kufanya vitendo visivyo sahihi.

"Katika kuendeleza soko letu ni lazima tuliopewa dhamana kusimamia sheria hizi na kutambua kuwa tuna dhima kubwa tuliyoaminiwa, hivyo tuitumie kwa uadilifu mkubwa," amesema.

Ashatu amewahimiza watumishi wa FCC kuwa waadilifu na weledi kwenye usimamizi wa sheria na kanuni zake ili kuwalinda walaji na wazalishaji.

"Mwenyekiti uadilifu na weledi ni muhimu zaidi kwenye kusimamia sheria na kanuni zake ili kuondokana na maumivu kwa mlaji, pia ombwe la kuwaumiza wazalishaji wanaonekana dhaifu kwenye soko," amesema Dk Ashatu.

Amesema Serikali jukumu lake ni kulea na kusimamia shughuli zote za uzalishaji na ushindani, kwa kutunga sheria zitakazohakikisha wafanyabiashara wote wanapata faida kupita njia sahihi na si za mkato.

"Katika masoko yetu kuna watu watumia njia mbalimbali kutaka kupata faida, kuna wanaopita njia halali na wanadumu kwa muda mrefu, lakini kuna wale wanaopita njia za mkato kutaka kuhodhi soko, jambo ambalo ni hatari kwa wengine," amesema.

Amesema watendaji na wadau katika sekta ya uzalishaji wanapaswa kuiishi kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo ‘Njama baina ya washindani na mathara yake kwa mlaji, ili kuendelea kulinda haki na usawa kwenye soko’.

“Nimuhimu kuendelea kutoa elimu kwa wadau na wazalishaji wenyewe na walaji ili kuelewana juu ya athari za kufifisha ushindani ndani ya Taifa letu, niipongeze FCC kwa kuzunguka katika kanda mbalimbali na kukutana na wadau na kuwapa elimu," amesema Dk Ashatu.

Kwa upande wake Dk Aggrey Mlinduka, Mwenyekiti wa Bodi wa FCC, pamoja na kuyapokea maagizo hayo na kuahidi kuzingatia uadilifu, amesema watazingatia haki katika kutekeleza wajibu wao wa kulinda ushindani ndani ya soko la Tanzania.

"Hatutaki kumuumiza mtu jukumu letu kuhakikisha watu wanazingatia sheria na kanuni, ili kama nchi tuwe na uchumi endelevu utakaosaidia kukuza ushindani wa ndani na nje," amesema.

Dk Mlimuka amemuomba waziri huyo kusaidia kutunga sheria zitakazowasukuma watendaji wa taasisi hiyo kutekeleza majukumu yao na kufikia maendeleo yanayotakiwa na nchi.

“Sheria ziwe kali kwa watendaji ili wawajibike tuondoe dhana kwamba wafanyakazi serikalini ni sehemu ya kumpumzika, mbona wakienda sekta binafsi wanafanya kazi na mafanikio yanaoneka," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live