Siku chache baada ya Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko kuagiza wafanyabiashara wa Madini kuacha kushusha ubora wa dhahabu (purity) katika Masoko ya Madini ametoa onyo kwa wote wanaojihusisha na vitendo hivyo kuacha mara moja.
Dk. Biteko, ametoa onyo hilo juzi katika Soko kuu la Dhahabu Mkoani Geita baada ya kufanya ziara ya kushtukiza wafanyabiashara na watumishi ili kubaini wanaoshusha ubora wa dhahabu katika soko hilo.
Amesema, Serikali itafuta leseni za wafanyabiashara wasio waaminifu wa madini ya dhahabu na hatua za kisheria zitafuatwa kwa wote wanaoshusha dhahabu katika masoko ya madini.
“Kitu cha kwanza tulichokubaliana tukibaini mmoja anafanya michezo hiyo tutakunyang’anya leseni ili ukafanye biashara nyingine ambayo unaweza kufanya ujanja ujanja, lakini biashara ya madini kila mtu tunataka afanye kwa haki, kulipa kodi yako sahihi, wateja wako uwalipe sahihi,” amesema Dk. Biteko.
Pia, ametoa onyo kwa maafisa wa Serikali wanaoshiriki katika mchezo huo wa kushusha ubora dhahabu. Amesema tayari wamekamilisha kupata orodha yao kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi.