Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dk Biteko: Safari matumizi nishati safi ya kupikia imeanza rasmi

Mkandarasi JNHPP Amelipwa Kwa Zaidi Ya Asilimia 80   Biteko Dk Biteko: Safari matumizi nishati safi ya kupikia imeanza rasmi

Fri, 8 Mar 2024 Chanzo: mwanachidigital

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema

safari ya matumizi ya nishati safi ya kupikia imeanza rasmi nchini.

Anasema huo ni utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuhakikisha wananchi hususan wanawake wa Tanzania wanahama kutoka kwenye matumizi ya nishati ya kupikia isiyo safi kwenda kwenye nishati safi na salama.

Dk Biteko amesema hayo leo Alhamisi, Machi 7, 2024, akiwa wilayani Temeke Mkoa wa Dar es

Salaam alikokabidhi mitungi ya gesi na majiko banifu kwa wajasiriamali wa Soko la Temeke Stereo na Mbagala- Zakhem.

“Nataka niwaeleze safari ya matumizi ya nishati safi ya kupikia imeanza wiki hii ambayo tunasherehekea Siku ya Wanawake Duniani, kwa sababu tunafahamu mwanamke ni mwathirika mkubwa wa nishati

isiyo safi ya kupikia na anapata madhara mbalimbali ikiwemo ugonjwa

wa kifua na kutumia muda mrefu kutafuta kuni,” amesema naibu waziri mkuu huyo.

Amesema kutokana na adha hiyo, Serikali

imeona ina wajibu wa kuweka mazingira wezeshi yatakayomsaidia mwanamke kupata nishati safi na kwa gharama nafuu.

Sambamba na hilo, Dk Biteko amewataka Watanzania kuacha tabia ya kukata miti ovyo na kuharibu vyanzo vya maji ambavyo baadhi hutumika kuzalisha umeme nchini.

“Nawaomba sana Watanzania tuwe na wivu na mazingira yetu, tulinde vyanzo vyetu vya maji,” amesema.

Akitaja mwarobaini wa changamoto hiyo, Naibu Waziri Mkuu Biteko amewahimiza Watanzania kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia kama ilivyo maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka nchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.

"Leo tumeanza na nyie kinamama katika kuhamasisha matumizi safi ya nishati ya kupikia, kesho tunahamia taasisi mbalimbali kama shule za bweni, magereza na hospitalini, tumeshatoa maelekezo huko, ili ziachane na matumizi ya kuni na mkaa,” ameeleza Dk Biteko.

Itakumbukwa, Rais Samia katika mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi ya Cop28 mwaka jana, alizindua Mradi wa Nishati safi ya kupikia kwa wanawake Afrika (AWCCSP), lengo ni kuendelea kuleta mageuzi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo ni mkombozi kwa mwanamke.

Agusia mgawo

Mbali ya hilo, Dk Biteko amesema changamoto ya mgawo wa umeme iko mwishoni kumalizika kwa sababu hivi sasa Serikali inaendelea na juhudi mbalimbali, ikiwemo ya kubadilisha miundombinu ya kusafirishia umeme ili iwe na uwezo wa kubeba umeme mwingi zaidi.

"Mfano kwa hapa Dar kutoka Kurasini hadi Ilala kuna waya za chini kwa chini umbali wa kilomita 6 za kusafirishia umeme, lengo ni kuhakikisha tunapata umeme tulivu na endelevu," amesema.

Awali, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema takwimu zinaonyesha hadi sasa kuna watu asilimia tano pekee wanaotumia nishati mbadala kama gesi nchini.

"Asilimia 63 wanatumia kuni, asilimia 25 wanatimia mkaa, kwa takwimu hizi bado tunasafari ndefu kama nchi, pia tunaweka juhudi kwa kushirikiana na wadau kama Oryx kuhakikisha tunahamia matumizi ya nishari safi hadi kufikia 2033 Watanzania wawe wamehamia kwa asilimia kubwa," amesema Kapinga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Oryx Tanzania, Benoit Araman amesema kupikia gesi kunaleta maendeleo kwenye jamii sambamba na kutunza mazingira kwa kuepusha kukata miti ovyo.

"Kutumia gesi kunalinda afya za wanawake, kwani kunawaepusha kuvuta hewa ya inayotokana na kuni pamoja na mkaa.

"Tunaendelea kutekeleza maagizo ya Serikali ya kwamba hadi ifikapo mwaka 2032, asilimia 30 ya Watanzania wawe wanatumia nishati bora ya kupikia," amesema Araman.

Mmoja ya kinamama wanufaika wa ugawaji mitungi hiyo, Beatrice Kagosi amesema hatua hii ni muhimu `kufikia malengo ya kuhamia katika matumizi ya nishati mbadala.

“Mimi kama mamalishe kuna muda vyakula vinapoa unawaza hadi uwashe tena mkaa, lakini mitungi hii unawasha na kupasha chakula,” amesema Kagosi.

Chanzo: mwanachidigital