Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Diplomasia ya uchumi ilivyoimarisha uhusiano wa Tanzania kimataifa

Uchumi Kupanda Diplomasia ya uchumi ilivyoimarisha uhusiano wa Tanzania kimataifa

Wed, 27 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baadhi ya wadau wa sekta ya habari, diplomasia na maendeleo ya kijamii wamechambua masuala kadhaa yaliyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Wameyataja kuwa ni kukuza diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa kimataifa, uhuru wa vyombo vya habari, sekta ya mazingira na siasa.

Wameeleza hayo jana Jumanne Machi 26, 2024 wakati wa mdahalo wa tathimini ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia aliyeingia madarakani Machi 19, 2021 baada ya mtangulizi wake hayati John Magufuli kufariki dunia Machi 17 mwaka huo. Mdahalo umeandaliwa na Taasisi ya Mchambuzi Media House Limited.

Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga amesema ndani ya miaka mitatu uhusiano wa Tanzania na mataifa mengine umeimarika.

Balozi Ulanga amesema ndani ya kipindi hicho Tanzania imefungua ofisi za ubalozi katika mataifa ya Indonesia na Australia ili kusogeza huduma karibu na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa mataifa hayo.

"Miezi mitatu au minne baada ya Rais kuingia madarakani, mlisikia tangazo la Denmark la kutaka kufunga ubalozi hapa, lakini miezi michache iliyopita mlisikia Denmark wamefuta uamuzi wao, haya ni mafanikio makubwa tunapaswa kujivunia,” amesema.

"Denmark na Tanzania zina uhusiano wa muda mrefu, uamuzi wao wa kufunga ubalozi haukuwa na ishara nzuri si wao tu, hata nchi zote za ukanda wa Scandinavia," amesema Balozi Ulanga.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu, Tanzania na mataifa mbalimbali yakiwamo ya Afrika Mashariki, yamekuwa na tume ya pamoja katika kuimarisha na kukuza ushirikiano.

Balozi Ulanga amesema ndani ya kipindi hicho, viongozi wa mataifa mbalimbali wametembelea Tanzania, wakiwemo marais na mawaziri wakuu.

"Ukiona viongozi wanapishana katika taifa lako ni dalili njema ya kuimarika kwa uhusiano," amesema.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu, amezungumzia uhuru wa vyombo vya habari katika kipindi cha miaka mitatu cha Rais Samia, akisema hatua kubwa imepigwa.

Amesema kiongozi huyo alipoingia madarakani alitaka kuwepo ushirikishwaji na kuvitambua vyombo vya habari.

"Hili lilitafsiriwa na wizara husika kwa kubadilisha dhana ya mwelekeo wa kuwa walezi wa vyombo vya habari, hapa mheshimiwa Waziri (Nape Nnauye) amejitahidi kusimamia vema mabadiliko ya sheria na kanuni, tunashirikishwa,” amesema na kuongeza:

"Kufunguliwa kwa magazeti ni hatua njema, lakini si yote yaliyorudi mtaani. Je yanatosha? Kwa sababu tunajenga nyumba moja ya vyombo vya habari huru itakayosaidia Taifa kuwa huru."

Machumu amesema kwa siku za usoni wangependa masuala hayo yawekwe katika mfumo wa sheria na kanuni ili kulinda tasnia hiyo, badala ya kutegemea utashi wa kisiasa au kiongozi aliye madarakani.

Mwanahabari mkongwe, Jesse Kwayu amesema uwajibikaji wa wanahabari na vyombo vya habari ni lazima.

Kwayu amesema haiwezekani kudai haki ya uhuru wa vyombo vya habari wakati hakuna uwajibikaji.

"Ili tujisimamie wenyewe lazima tuwajibike kwa sababu ni dhima kubwa ya kuhakikisha Taifa linasonga mbele," amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Joyce Shebe amezungumzia masuala ya mazingira, hasa katika mabadiliko ya tabianchi akisema Rais Samia amelipa uzito unaostahiki katika kukabiliana nalo.

"Kuna utashi wa kisiasa na Rais Samia ameonyesha nia ya kukabiliana na suala hili, ameshiriki mikutano mikubwa kuhusu tabianchi," amesema Shebe.

Mdau mwingine, Dk Dennis Muchunguzi amesema kwa siku za usoni kuwe na siasa safi zitakazohakikisha vyama vinakuwa imara kifedha, si visiwepo baada ya muda vinapotea.

Amesema pia kuwe na haki sawa itakayotambua sekta binafsi ni nguzo ya kiuchumi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live