Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dewji mkurugenzi bora Afrika, METL muuzaji bora Afrika Mashariki

28803 DEWJI+PIC TanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Mohammed Dewji akishinda tuzo ya mkurugenzi bora Afrika, kampuni yake, Mohammed Enterprises Limited (Metl) imetajwa kuwa kinara wa usafirishaji Afrika Mashariki.

Tuzo ya Dewji imetolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Africa Investments Forum and Awards (AIFA) huku Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), ikiizawadia Metl kuwa kinara wa usafirishaji wa bidhaa za Tanzania ukanda wa Afrika Mashariki.

Ni kwa kuiongoza vyema Metl, Dewji amepata tuzo hiyo inayoandaliwa na Leaders League ya Ufaransa. AIFA hutoa tuzo kwa kampuni zinazojihusisha na uchimbaji madini, nishati, miundombinu na upangaji miji na nyumba na makazi.

Ili kuhamasisha uuzaji nje wa bidhaa za Kitanzania, TCCIA imezindua mashindano yatakayokuwa yanatoa tuzo kwa kila msafirishaji bora.

Kwa kuanza, mwaka huu imewatunukia washindi 10 kwenye maadhimisho ya miongo mitatu tangu kuanzishwa kwake.

“Tunazo rasilimali nyingi sana nchini, kinachohitajik ani kuzitumia fursa zilizopo. Fursa haziwezi kukutafuta ni lazima uchangamke, ukijituma mafanikio yapo,” amesema Shubash Patel ambaye alikuwa mgeni rasmi wa tuzo hizo.

Patel ambaye ni mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) amesisitiza: “Tukope na kulipa kwa wakati, tukiwa waaminifu, Tanzania ya viwanda inawezekana.”

Mwishoni mwa wiki iliyopita, washindi walitangazwa na kupewa tuzo zao. Washindi hao walikuwa kampuni za Said Bharessa zilizoshinda kwa kuuza zaidi soko la Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) na Mohammed Entreprises Limited (Metl) walioongoza Afrika Mashariki.

Wengine walikuwa kampuni ya Prince Africa kinara wa kusafirisha bidhaa za pastiki nje ya nchi wakati kampuni ya Kioo ikiongoza kwa kusafirisha vifungashio na Kwanza Collections wakishamiri kwenye bidhaa za ubunifu.

Tanzania Leaf Tobacco Industries waliongoza kwenye usafirishaji wa mazao ya biashara huku kampuni ya Export Tradin Group ikipata tuzo ya usafirishaji wa mazao ya chakula na Tanzania Distillers wakiongoza kwa usafirishaji wa vinywaji.

Kampuni ya Alaf imenyakua tuzo ya usafirishaji wa vifaa vya ujenzi huku kampuni ya Agreko ikipata tuzo ya mwanamke aliyesafirisha zaidi.

Meneja masoko, mawasililiano na uhusiano wa Benki ya KCB ambayo ilikuwa mdhamini mkuu wa tuzo hizo, Christine Manyenye amesema wanawake ni warejeshaji wazuri wa mikopo kuliko wanaume.

“Kwa utafiti wetu, wanawake wanarejesha zaidi kuliko wanaume hivyo tumewaandalia utaratibu maalumu. Tunawafundisha kisha wataalamu wetu wanawasaidia kurasmisha biashara zao,” amesema Christina.

TCCIA ilianzishwa mwaka 1988 na imekuwa muhimu kwa wauzaji wa bidhaa nje ya nchi.  Makamu wa rais wa TCCIAOctavian Mshiu amesema tuzo hizo zitaendelea kutolewa kila mwaka.

“Sisi ndiyo tunaotoa cheti cha asili ya bidhaa. Usafirishaji wa bidhaa unasaidia kuimarisha urari wa biashara na thamani ya sarafu,” amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz