Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Deni la Sh43 milioni laifanya Tanesco kukata umeme mamlaka ya maji Serengeti

90415 DENI+PIC Deni la Sh43 milioni laifanya Tanesco kukata umeme mamlaka ya maji Serengeti

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Serengeti. Wakazi wa mji wa Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara nchini Tanzania wanafunga mwaka 2019 na kufungua mwaka 2020 bila huduma ya maji kufuatia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)  kuwakatia Muguwasa umeme kwa kudaiwa kutolipa deni la Sh43 milioni wanalodaiwa.

Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mugumu (Muguwasa) imekuwa kwenye mgogoro wa muda mrefu na Tanesco kutokana na kulimbikiza madeni na kila mwezi wamekuwa wakikata umeme kushinikiza malipo na kusababisha adha kubwa kwa wananchi.

Kaimu fundi mkuu wa Tanesco wilaya hiyo, Peter Mtete leo Jumanne Desemba 31,2019 ameliambia Mwananchi wamesitisha huduma ya umeme kuanzia jana Jumatatu baada ya kuwakumbusha bila mafanikio.

"Kabla ya Muguwasa kuhamia Wakala wa Maji vijijini walikuwa na deni la Sh20 milioni ambazo walikuwa wanalipa kwa pamoja na Halmashauri ya Wilaya, toka Julai mpaka sasa deni limefikia Sh23 milioni na kufanya deni zima kuwa Sh43 milioni," amesema.

Amesema malipo waliyoona kwenye mfumo ni Sh3 milioni, lakini hawataweza kufungua huduma ili waweze kulipa  kwa kuwa awali walikuwa wanasingizia kuwa gharama wanazotoza za maji ni ndogo lakini wamepandisha kwa asilimia 50 hakuna mabadiliko.

"Wanadai wana wateja 1500  kati ya wakazi zaidi ya 35,000 wa mji huo ambao walikuwa wanawatoza Sh7,500 sawa na Sh11,250,000 kwa mwezi, umeme ni Sh9-10 milioni lakini wanashindwa kulipa hata kidogo, wamepandisha gharama hadi Sh12,000 kwa mtu mwenye matumizi madogo ambapo wanaweza kusanya Sh18 mil lakini hakuna mabadiliko, sisi tunatekeleza agizo la Rais la maneno mawili tu KA TA," amesema.

Kaimu meneja wa Muguwasa, Charles Msiba amekiri kusitishwa huduma ya umeme kutokana na deni na kudai kuwa ameishalipa Sh3 milioni na sasa anaandaa malipo mengine ya Sh3 milioni na deni litabaki Sh37 milioni.

"Changamoto kubwa ni ubovu wa miundombinu ya mwaka 1975 hairuhusu kuongeza wateja na unachangia gharama kubwa za uendeshaji kutokana na kuharibika mara kwa mara, pia wateja wetu wanalipa kwa kusuasua sana," amesema.

Amesema kwa sasa wanategemea mapato yao yatapanda na kuwawezesha kupunguza deni na kuwalipa watumishi wao.

Chanzo: mwananchi.co.tz