Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Deni la Sh42 bilioni, lazuia kasi ya Temesa

Fedhapic Deni la Sh42 bilioni, lazuia kasi ya Temesa

Sat, 9 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Musoma. Deni la Sh42 bilioni, ambalo Serikali na taasisi zake wanadaiwa na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), limeelezwa kuwa kikwazo cha utendaji kazi wa wakala huo.

Deni hilo linatokana na malimbikizo ya malipo kutokana na huduma ambazo wakala huo ulizitoa kwa Serikali na taasisi zake hadi kufikia Julai 30 mwaka huu.

Hayo yamebainishwa Ijumaa Desemba 8, 2023 na Mtendaji Mkuu wa Temesa, Lazaro Kilahala kwenye mkutano wa wadau wa wakala huo, uliofanyika Musoma mjini.

"Tayari ipo mikakati kadhaa ambayo tumeifanya ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha ili kuangalia namna gani taasisi hizo zinalipa madeni hayo, na huu pia ni moja ya mkakati wa maboresha ya utendaji kazi wa wakala," amesema.

Amesema wakala huo tayari umeanza kufanya maboresho mbalimbali kwenye huduma zake kufuatia kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wateja na wadau wake juu ya utoaji wa huduma usioridhisha.

Miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja na kuingia mkataba na baadhi ya viwanda vinavyozalisha vilainishi na vifaa vya umeme nchini, hatua ambayo imesaidia upatikanaji wa haraka wa vifaa hivyo na kwa bei nafuu, tofauti na awali ambapo walikuwa wakinunua kwa wafanyabiashara wa kawaida.

"Gharama kubwa, ucheleweshaji wa kazi na vipuri feki ni miongoni mwa malalamiko yaliyokuwepo, sasa mbali na kuingia mkataba na viwanda pia tumeingia mkataba na wazabuni wanaotuletea vipuri vya magari na endapo mzabuni ataleta kifaa feki gharama itakuwa juu yake na ikitokea amefanya hivyo zaidi ya mara mbili, tunavunja mkataba.

"Tangu tumeanza utaratibu huu Agosti, 2022 hatujapata kesi yoyote ya kifaa feki na tunataka kuhakikisha huduma zetu zinakuwa bora zaidi, ambapo mnufaika mkuu wa matokeo haya ni mwananchi kwani viongozi wa Serikali watakuwa na uwezo wa kuwafikia kwa haraka na usalama zaidi,”amesema.

Kwa upande wa Meneja wa Temesa mkoani Mara, Joseph Rigate amesema wakala huo unadai zaidi ya Sh300 milioni kutoka kwa taasisi za umma na Serikali mkoani humo.

"Tumeamua kubadilika kiutendaji na tunataka kutoa huduma bora yenye viwango kwa gharama nafuu lakini suala la madeni ni kikwazo, kwani kuna wazabuni tunatakiwa kuwalipa kwa wakati ili waweze kuendelea kutuhudumia.

“Tunaziomba hizi taasisi zilipe madeni yao," amesema.

Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dk Halfan Haule amezitaka taasisi zote zinazodaiwa kulipa madeni yao ili kuiwezesha Temesa kufanya shughuli zake kwa ufanisi.

"Kulikuwa na changamoto huko nyuma lakini sote ni mashahidi tumeona namna ambavyo Temesa inajitahidi kuboresha huduma, tusiwe kikwazo tulipe madeni yetu haraka iwezekanavyo.

"Ni kweli kuna mabadiliko makubwa Temesa, maboresho haya yaendelee ili wateja tupate huduma bora zenye hadhi na zinazolingana na bei ya soko, hii itajenga imani kwa wateja na kuwa na moyo wa kuendelea kupata huduma Temesa, " amesema Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Michael Mtenjele.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live