Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Darcoboa watoa suluhisho ongezeko la nauli

Gesi Magari Tanzania Darcoboa watoa suluhisho ongezeko la nauli

Thu, 30 Nov 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Mabrouk Sabri amesema suluhu ya kutokupanda nauli mara kwa mara ni kuanza kutumia nishati mbadala.

Kauli hiyo ameitoa leo Novemba 29, 2023 wakati akichangia mada katika mjadala wa uliokuwa na mada ya ‘Nini maoni yako kuhusu mabadiliko ya nauli ya mabasi, Daladala’.

Katika maelezo yake Sabri ameitaka Serikali kuangalia namna ya kubadili mifumo ya mabasi kwenda kwenye gesi asilia.

“Suluhu ya nauli kutokupanda mara kwa mara ni kutumia nishati mbadala. Ukipita mitaani madereva taxi wamefunga gesi na wanatoa ushuhuda gharama zimepungua, yapo pia mabasi ya shule yaliyofungwa mifumo ya gesi,” amesema.

Sabri amesema kutokana na gharama za uendeshaji kupanda, hata kiwango cha nauli kilichopanda bado ni kidogo na si rafiki kwao, kwani wao walikuwa wanatamani kupanda kutoka Sh500 iwe Sh800 ingeleta nafuu kwao.

“Kwa bahati mbaya sana watu wanaangalia gharama za mafuta, lakini vipuri vyote kwenye magari yetu yanaagizwa kutoka nje na ukiangalia dola ipo juu ya fedha yetu imeshuka thamani,” amesema.

Kwa upande wake mtumia usafiri, Adrew Mseya amesema, “Ninachokiona ifike mahala jamii ipewe elimu kwanza mambo gani yanayoweza kupandisha nauli ndipo hatua zichukuliwe sasa imekuwa taharuki,”amesema.

Hata hivyo, Meneja Leseni Udhibiti Usafiri wa Barabara (Latra), Leo Ngowi ameeleza mchakato uliofanyika hadi kutangazwa kwa ongezeko la nauli, ikiwemo kupokea maoni ya watoa huduma wote nchini kufanya wasilisho kueleza sababu ya ongezeko hilo.

“Mamlaka baada ya kusikiliza wananchi, tulikwenda kufanya utafiti na tulipeleka maandiko Serikalini na chapisho hilo kutolewa juzi.

“Waliotoa maoni waliomba ongezeko kubwa zaidi, hivyo tulikwenda kuangalia gharama halisi ya shilingi kwa sasa na gharama ya vipuri na uwezo wa wananchi kulipa,” amesema.

Amesema nauli zilizopandishwa zimezingatia gharama za maisha na uwezo wa wananchi.

“Nauli hizi tumeziweka ili mtoa huduma asikwame, baada ya miaka 10, aweze kununua chombo kingine na huduma iwe endelevu,

“Ukiangalia kwenye sekta yetu tusipochangia kwa uwazi tutakuja kuwa na usafiri wa bajaji mijini kwa kiasi kikubwa kwasababu zimeendelea kuongezeka kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Chanzo: mwanachidigital