Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesema Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa kusajili miradi ya uwekezaji mwezi uliopita. Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Gilead Teri alieleza hayo katika Ripoti ya Uwekezaji ya TIC kwa mwezi uliopita.
Teri alisema kati ya miradi 37 ya uwekezaji iliyoidhinishwa na kusajiliwa TIC mwezi uliopita, miradi 20 itawekezwa kwenye Mkoa wa Dar es Salaam na inatarajiwa kuzalisha ajira 5,395. “Miradi hii inatarajiwa kuwa na uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 672.44 (Sh trilioni 1.581) sawa na asilimia 84 ya uwekezaji wote wa miradi 37,” alisema Teri.
Aliitaja mikoa mingine iliyovutia uwekezaji kwa mwezi uliopita kuwa ni Dodoma miradi miwili yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5.57 (Sh bilioni 13.1) itakayozalisha ajira 199, Iringa miradi miwili yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 72.5 (Sh bilioni 170.68) itakayozalisha ajira 400 na Kilimanjaro miradi miwili yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 6.95 (Sh bilioni 16.3) itakayozalisha ajira 305.