Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dar-Moro kwa SGR kuanza Agosti

22fcd47b76d7d8a716a0a116a419cc47 Dar-Moro kwa SGR kuanza Agosti

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho amesema usafiri wa treni ya mwendo kasi kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro utaanza rasmi Agosti mwaka huu na sasa kinachosubiriwa ni kuwasili kwa treni za umeme kwa ajili ya kuanza majaribio.

Alisema hayo juzi wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyokuwa ikikagua ujenzi wa reli ya SGR kuanzia stesheni ya Ihumwa- Dodoma hadi Stesheni ya Morogoro.

Waziri alisema ujenzi kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 huku ile ya kutoka Morogoro hadi Makutupora Dodoma imefikia asilimia 50.

"Mwezi Juni tunatarajia kupata treni ya umeme na tutaifanyia majaribio na Agosti treni itaanza rasmi kufanya kazi, mwakani, treni kutoka Morogoro hadi Makutupora -Dodoma itaanza kufanya kazi baada ya kukamilika,” alisema.

Kamati ya Bunge ya Miundombinu na wabunge ambao ni wajumbe wa kamati wameridhishwa na ujenzi unaoendelea na hatua iliyofikiwa

Alisema katika Afrika kwa ujumla reli ya SGR inayojengwa nchini ndiyo bora na inaweza kuhimili mzigo mzito wa tani 35.

"Wenzetu reli yao inahimili tani 25 tu lakini sisi ni tani 35 maana yake unaweza kubebesha behewa juu ya behewa," alisema.

Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Reli Tanzania ( TRC ), Profesa John Kondoro alisema ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na kazi nzuri imefanyika.

Alisema hadhi ya madaraja ni nzuri jambo linaloonesha yatadumu kwa muda mrefu. Kondoro alisema kufikia Julai mwaka huu, vichwa vya treni na mabehewa yatakuwa yamefika .

"Safari ya kwanza kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro itakuwa imekamilika. Dar es Salaam kuna sehemu za kukamilisha kati ya Buguruni na Ukonga,"alisema.

Alisema uwepo wa SGR utafanya Tanzania kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso alishukuru serikali kwa kujenga SGR akisisitiza kuna maendeleo makubwa yanafanyika. “Hata yale mambo tuliyokuwa tukishauri bungeni yamefanyiwa kazi," alisema.

Kaimu Meneja Msaidizi wa Mradi kutoka stesheni ya Morogoro, Mhandisi Simon Mbaga alisema ujenzi wa stesheni Morogoro umefikia asilimia 98 na wako katika hatua ya mwisho ya utekelezaji.

Alisema itakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 185 watakaokuwa wamekaa na zaidi ya abiria 400 wanaweza kuhudumiwa kwa wakati mmoja. Stesheni itakuwa na vioski vitano, mighahawa minne na itakuwa na uwezo wa kuegesha magari madogo 180, mabasi sita na malori matano.

Chanzo: www.habarileo.co.tz