Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Dangote yaahidi makubwa uzalishaji saruji

13049 Pic+dangote TanzaniaWeb

Tue, 21 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara kinatarajia kuongeza kiwango cha uzalishaji mara tatu zaidi kutoka wastani wa tani 2,000 za sasa kwa siku hadi tani 6,000.

Uzalishaji huo utakaoanza siku 30 zijazo kuanzia jana, imeelezwa utatokana na ongezeko la megawati 35 za umeme utakaozalishwa kwa kutumia gesi asilia ikilinganishwa na wastani wa megawati 20 zilizotokana na matumizi ya lita 106,000 za dizeli kwa siku.

Hilo likifanyika litaongeza saruji sokoni na kuwezesha bidhaa hiyo kushuka bei.

Hayo yalielezwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, Jagat Rathee jana, wakati wa kusaini mkataba wa miaka 20 na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa ajili ya kuwaunganishia gesi asilia kiwandani hapo.

Makubaliano hayo yalisainiwa jijini Dar es Salaam kati ya TPDC na uongozi wa kiwanda hicho kinachomilikiwa na mfanyabiashara tajiri barani Afrika, Aliko Dangote.

“Tunategemea kiwango cha uzalishaji kuongezeka kutokana na gharama ndogo za uzalishaji kwa njia ya gesi,” alisema Rathee.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Kapuulya Musomba alisema kiwanda hicho ni kati ya saba vilivyopo kwenye mpango wa shirika hilo wa kupatiwa gesi katika mwaka wa fedha wa 2018/19.

“Tunajua Serikali iko katika hatua za kujenga uchumi wa viwanda, kwa hiyo TPDC kwa nafasi yetu tutahakikisha viwanda vinazalisha bidhaa kwa gharama nafuu kupitia matumizi ya gesi,” alisema.

Alisema wataanza kutumia futi za ujazo milioni nane na baada ya miaka miwili ijayo watatumia futi za ujazo milioni 20.

Musomba alisema kiwanda hicho kinaongeza idadi ya viwanda vinavyotumia futi za ujazo milioni 15 tu ya gesi asilia katika uzalishaji kufikia 42 wakati akiba ya gesi asilia hadi sasa ni futi za ujazo trilioni 57.

Makubaliano hayo yamefikiwa ikiwa ni siku chache baada ya Serikali wiki iliyopita kukubaliana na wadau wa saruji kuhakikisha kuwa bidhaa hiyo inapatikana sokoni kwa uhakika na bei inashuka.

Pia walikubaliana kampuni ya Tancoal ambayo ni wazalishaji wakuu wa makaa ya mawe wahakikishe yanapatikana kwa wingi kwa ajili ya viwanda vya ndani kabla ya kuuzwa nje.

Baadhi ya wazalishaji wa saruji walisema upatikanaji mdogo wa makaa ya mawe ni chanzo cha uhaba wa saruji nchini, jambo lililosababisha kuadimika kwa bidhaa hiyo na kupanda bei sokoni.

Chanzo: mwananchi.co.tz