Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wanatengeneza miundombinu mizuri na kuwapatia Wavuvi wanaoishi kandokando ya ukanda wa Ziwa Tanganyika na maeneo mengine vifaa vya kisasa vya uvuvi ili viwasaidie kuongeza thamani ya zao la Dagaa na kupunguza upotevu wa zao hilo baada ya kuvua.
Ulega aliyasema hayo wakati wa ziara yake aliyoifanya katika vijiji vya Buhingu na Katumbi vilivyopo wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma Mei 6 - 7, 2022.
Wakati akiongea na Wavuvi wa vijiji hivyo kwa nyakati tofauti alisema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kukuza uchumi wa buluu na ndio maana inatengeneza miundo mbinu mizuri ya kuchakata dagaa na mazao mengine ya samaki ili kuwaongezea thamani na waweze kuuzika kwa bei nzuri na wananchi wafaidike na zao hilo.
"Tunataka tuone zao la dagaa ambalo huku kigoma linazalishwa kwa wingi linainua maisha ya watu, hatutaki kuona hata dagaa mmoja anapotea kwa kuharibika au kuoza, lengo letu ni kuona ukanda wote huu wa Ziwa Tanganyika mnanufaika ipasavyo kupitia dagaa", alisema
Aliongeza kuwa wanawapatia Wavuvi hao vifaa ikiwemo Boti, injini, nyavu, kamba na taa lengo likiwa ni kufanya Uvuvi endelevu na kulifanya zao la Dagaa kuwa la kimkakati ili liwe chachu ya maendeleo kwa wavuvi hapa nchini.
"Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo tunaendelea kutengeneza miundombinu mizuri ya kuchakata dagaa na mazao mengine ya samaki katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kupunguza upotevu wa mazao hayo na kuyaongezea thamani ili yauzwe kwa bei nzuri ndani na nje ya nchi", alifafanua
Aidha, aliwataka wananchi wanaoishi kandokando ya ukanda wa Ziwa Tanganyika kuendelea kutunza na kuhifadhi mazalia ya samaki ili uvuvi katika eneo hilo uwe endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mhe. Hanaf Msabaha alisema kuwa kuna haja Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuanzisha miradi ya ufugaji wa samaki Wilayani humo ili samaki waweze kupatikana muda wote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mradi wa Tuungane ambao unatekelezwa Mkoani Kigoma, Bw. Lukindo Hiza alisema tayari wameshirikiana na Uongozi wa Wilaya ya Uvinza kwa ajili ya kujenga Mwalo wa kisasa utakaosaidia kupunguza upotevu wa dagaa na wataweza kuwaongezea thamani ili wawauze kwa bei nzuri zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.