Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DPP asimamia mwenyewe maombi ya kutaifisha mabilioni ya DECI

50115 Decipic

Wed, 3 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imesikiliza maombi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ya kutaifisha mali za kampuni iliyokuwa ikiendesha biashara ya upatu ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI), zikiwemo pesa taslimu Sh14.1 bilioni.

Maombi hayo yamesikilizwa na Jaji Stephen Magoiga leo, Jumanne, April 2, 2019, huku DPP Biswalo Mganga akiongoza mwenyewe jopo la mawakili watatu wa Serikali kuhakikisha mali na mabilioni hayo ya pesa yanakuwa mali ya Serikali kwa mujibu wa sheria, kwa matumizi ya umma.

DPP amefungua maombi hayo mahakamani hapo ikiwa ni miaka takribani sita baada viongozi wa kampuni hiyo ya DECI kutiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika kesi ya jinai namba 109 ya mwaka 2009, kwa kosa la kuendesha biashara ya upatu, kinyume cha sheria.

Viongozi hao wa DECI, ambao walikuwa wachungaji na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Kipentekoste, walitiwa hatiani kwa kosa hilo mwaka 2013 na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya jumla ya  Sh21 milioni. Walilipa faini hiyo na hivyo wakaepuka kifungo.

Waliotiwa hatiani katika kesi hiyo, ambao ndio wajibu maombi katika maombi ya DPP ni Jackson Sifael Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Saigaran ole Loitginye na Samwel Sifael Mtares.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro aliieleza Mahakama kuwa wajibu maombi walishatiwa hatiani katika kesi ya jinai namba 109 ya mwaka 2009, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa kosa la kuendesha shughuli za upatu.

Wakili Kimaro alibainisha kuwa kosa hilo ni moja ya makosa makubwa na kwamba msimamo huo ulishatolewa hata na Mahakama ya Rufani katika rufaa ya DPP kupinga uamuzi wa mahakama za chini kuwarejeshea pesa zao waliokuwa wamewekeza amana zao.

Alisema kutokana na uzito huo wa kosa hilo, Mahakama ya Rufani pia ilielekeza DPP afungue maombi Mahakama Kuu ya kutaifisha mali zote zilizopatikana kutokana na kosa hilo.

Huku akirejea kesi mbalimbali zilizokwisha kuamuriwa na mahakama za ndani na za nje ya nchi, Wakili Kimaro alisema suala la kutaifisha mali zilizotokana na kosa la uhalifu si jipya na lengo ni mhalifu asinufaike na uhalifu huo.

Alidai wana ushahidi wa kutosha kwamba mali hizo walizoziorodhesha katika maombi hayo zikiwemo pesa hizo zimetokana na kosa hilo, huku akirejea utetezi wa baadhi ya wajibu maombi kuwa hawakuwa na biashara nyingine zaidi ya upatu.

Wakili Kimaro alisisitiza hata katika kiapo chao kinzani hawajaeleza chanzo kingine cha mali hizo.

Kwa upande wake Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alisisitiza uamuzi wa kesi hizo walizozirejea za ndani na nje unasisitiza kuwa wahusika wasiweze kufaidika na mapato ya mali hizo zilizotokana na kosa la uhalifu.

Mahakama baada ya kusikiliza hoja za upande wa DPP imeahirisha usikilizwaji huo hadi saa 10 jioni itakapoendelea na usikilizwaji wa hoja za wajibu maombi wanaowakilishwa na Wakili Majura Magafu.

Awali Jaji Magoiga alitupilia mbali maombi ya wahanga 18 wa DECI waliokuwa wakiomba walipwe jumla ya Sh2.4 bilioni kutoka katika Sh14.1 bilioni za DECI ambazo Serikali ilizuia katika akaunti za benki mbalimbali, tangu mwaka 2009, baada kuwashtaki viongozi hao wa DECI  na kutiwa hatiani.

Walifungua maombi hayo siku chache tu baada ya DPP kufungua maombi mahakamani hapo akiomba mahakama iamuru kutaifishwa kwa mali mbalimbali za kampuni hiyo ya DECI zikiwemo pesa taslimu Sh14.1 bilioni, nyumba, viwanja na magari ya kifahari.

Katika maombi yao walikuwa wakidai kuwa walikuwa wameweka amana zao katika kampuni hiyo ili baadaye wapate faida, kwa mtindo waliokuwa wakiuita wa kupanda mbegu na kisha kuvuna, kiasi cha Sh300,000 kila mmoja na kwamba kila mmoja alishalipwa viwango mbalimbali vya fedha.

Hivyo walikuwa wakidai wote kwa pamoja walipwe jumla ya Sh2.4 bilioni katika fedha hizo ambazo DPP anaomba mahakama iamuru zitaifishwe na Serikali.

Hata hivyo Jaji Magoiga ameyatupilia mbali maombi hayo baada ya kubaini kuwepo na kasoro ya kisheria katika hati ya kiapo iliyokuwa inaunga mkono maombi yao kutokana na kutokuwa na tarehe.

Akitoa uamuzi wake Jaji Magoiga amesema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 8 cha Sheria ya Viapo, ni lazima kiapo kionyeshe tarehe na mahali kilikotolewa.

“Maombi haya namba 65 ya mwaka 2019 yanakiuka sheria. Kwa msingi huo ninayatupilia mbali.”, alisema Jaji Magoiga.

Washtakiwa hao sita kati ya 18 ambao ni pamoja na Andrew Tungaraza, Frida Msuva, Imelda Adolph, Jackson Nyera, Tadea Mgoso na Philemon Mwarko, juzi walikamatwa na polisi baada ya kutoka mahakamani na kwenda kuhojiwa kabla ya kuachiwa.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz