Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DNA ya mazao kuwabana wafanya biashara mipakani

Mazao Wa Kike DNA ya mazao kuwabana wafanya biashara mipakani

Wed, 21 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mamlaka ya afya ya mimea na viuatilifu Tanzania (TPHPA), imeanza kutumia teknolojia mpya ya vipimo vya vinasaba (DNA) kwa ajili ya utambuzi wa mazao na bidhaa za kilimo zinazozalishwa nchini, ili kudhibiti wafanya biashara wasio waaminifu.

Teknolojia hiyo iliyoanza kutumika kwenye mpaka wa Namanga mkoani Arusha, imeonyesha mafanikio makubwa na itasambazwa katika vituo vyote vikubwa vya ukaguzi vya TPHPA.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Februari 21, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru alipokuwa akitoa maelezo kwa Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu alipotembelea makao makuu ya mamlaka hiyo jijini hapa.

Profesa Ndunguru amesema mashine hiyo yenye uwezo pia wa kupima viumbe hai, itasaidia nchi kudhibiti udanganyifu wa biashara za mazao ya kilimo unaofanyika mipakani, kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutoa taarifa sahihi ndani ya dakika 20 ya bidhaa husika inatoka nchi gani.

“Kuna baadhi ya wafanya biashara hukwepa kodi kwa kudanganya, mfano anataka kusafirisha mchele au mahindi nje ya nchi au anataka kuingiza nchini, anadanganya bidhaa hiyo ni ya Tanzania ili asilipie kodi kumbe ni ya nchi nyingine, mashine hii itaonyesha ndani ya dakika 20 na muhusika ataumbuka na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesema Profesa Ndunguru.

Lengo la kuanza kutumia teknolojia hiyo, Profesa huyo amesema mbali ya kudhibiti mapato ya nchi, lakini pia itasaidia kulinda afya za walaji wa bidhaa zinazotoka nchini kwenda nchi zingine na zinazoingizwa nchini.

“Lengo lingine ni kujua mwenendo wa biashara za mazao ya kilimo ya Tanzania zinakwenda wapi hasa na bidhaa zipi zinaingia sana nchini, ili kulinda masoko yetu na kufungua mapya katika nchi mbalimbali kwa ajili ya uchumi wa Taifa,” amesema.

Awali, akizungumzia ziara yake, Mchechu amesema lengo ni kuzipitia taasisi za umma kuona utekelezaji wa majukumu yao, maendeleo yake na changamoto wanazopitia ili kuona namna ya kushirikiana kuzitatua ili kuboresha utendaji kazi wao.

“TPHPA ni moja ya taasisi muhimu nchini hasa katika kuimarisha uchumi wa wakulima na wafanya biashara wa mazao, lakini pia ndio mhimili mkuu wa usalama wa chakula, hivyo tumekuja kuwatembelea kuona utendaji kazi wao lakini pia mambo yanayowatatiza ili kuunganisha nguvu kutatua kwa ajili ya kusongesha mbele gurudumu hili la maendeleo,” amesema Mchechu.

Hata hivyo, amesema changamoto kubwa waliyoiona katika mamlaka hiyo ni uhaba wa watumishi lakini pia rasilimali fedha katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kitafiti na ukaguzi.

“Nakwenda kuanza na changamoto hizo mbili lakini niwapongeze kwa kuwa changamoto hizo hazijakwamisha ufanisi wa kazi.”

Nitumie nafasi hii kuzitaka taasisi zingine kuwa na mtazamo chanya wa kujikwamua na changamoto kusudi zisiathiri utekelezaji wa majukumu yao,” amesema Mchechu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live