Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DMI kujenga vyuo viwili vya ubaharia Mwanza, Lindi

BAHARIA TAALUMA DMI kujenga vyuo viwili vya ubaharia Mwanza, Lindi

Sun, 25 Jun 2023 Chanzo: Mwananchi

Chuo cha Ubaharia Dar es Salaam (DMI) kinatarajia kujenga vyuo vipya viwili katika mikoa ya Mwanza na Lindi kwa lengo la kupanua na kufikisha huduma karibu na wananchi.

Mwenyekiti wa Bodi ya DMI, Kapteni Ernest Bupamba amesema kwa Mkoa wa Mwanza, chuo hicho kitajengwa Wilaya ya Ilemela ambako tayari kiwanja kimepatikana huku kwa Mkoa wa Lindi, chuo kipya kitajengwa Wilaya ya Kilwa. Akizungumza na Mwananchi katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza ambako maadhimisho ya siku ya Ubaharia duniani yanaendelea, Kapteni Bupamba amesema miradi hiyo miwili ni utekelezaji wa mikakati ya chuo hicho kusogeza huduma zake sehemu tofauti nchini.

‘’Kwa sasa, huduma zote za mafunzo za DMI zinapatikana jijini Dar es Salaam na wakati mwingine katika maeneo maalum kulingana na mahitaji, ujenzi wa vyuo katika mikoa ya Mwanza na baadaye Lindi utatanua huduma zetu katika maeneo mengine. Tutaendelea kujenga vyuo katika mikoa mengine kadri mahitaji na uwezo,’’ amesema Kapteni Bupamba bila kutaja gharama zitazotumika Amesema taasisi ya DMI siyo tu itaendelea kujenga vyuo katika maeneo tofauti nchini, bali pia kusimamia misingi ya utoaji wa elimu bora kuwezesha mabaharia wa Kitanzania kuwa na stadi, ujuzi na maarifa yanayokidhi mahitaji ya soko la ubaharia duniani. Akizungumzia mazingira na maslahi bora kwa mabaharia, Katibu Chama cha Mabaharia Zanzibar, Hussein Uki ameiomba Serikali kukamilisha mchakato wa kuandaa skimu ya kazi ya kada hiyo kuwaondolea mabaharia adha ya malipo duni licha ya umuhimu wao katika uchumi na maendeleo duniani. ‘’Zaidi ya asilimia 90 ya mizigo yote duniani husafirishwa kwa njia ya maji, na kazi hiyo hufanywa na mabaharia ambao mazingira na maslahi yao bado ni duni. Serikali lazima iboreshe mazingira ya kazi na maslahi ya mabaharia,’’ amesema Uki Suala la mikataba ya ajira kwa mabaharia wa Kimataifa, hasa kwenye meli za Kimataifa zinazopeperusha bendera ya Tanzania ni eneo lingine muhimu ambalo kiongozi huyo wa Mabaharia nchini ameiomba Serikali kutupia macho kutokana na ukaidi wa baadhi ya meli hizo kutoairi Watanzania. ‘’Mabalozi wa Tanzania nje ya nchi pia watumike kutafuta fursa za ajira katika fani ya ubaharia kwa ajili ya Watanzania. Wenzetu katika nchi jirani wanafanya hivyo kuwanufaisha mabaharia wao,’’ amesema Uki Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi Zanzibar, Suleiman Masoud Makame ameziagiza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), Mamlaka ya Usafiri wa Baharini ya Zanzibar (ZMA) na taasisi zingine zinazohusika kuhakikisha mabaharia wanapata mazingira na maslahi bora kazini. ‘’Tasac na ZMA zitimize wajibu kusimamia mazingira bora ya kazi kwa mabaharia, likiwemo suala la mabaharia wanawake kupata maeneo au vyumba maalum vya faragha wawapo kazini,’’ amesema Waziri Makame Akitoa elimu kwa umma unaotembelea vibanda vya taasisi na wadau wa sekta ya usafirishaji majini vilivyoko viwanja vya Furahisha jijini Mwanza, Meneja mafunzo na utoaji vyeti kutoka Tasac, Lameck Sondo amewaomba Watanzania kuacha tabia ya kutupa taka ngumu ndani ya mito, maziwa na bahari ili kulinda mazingira, usalama wa vyombo na abiria. ‘’Taka ngumu zinazotupwa ndani ya mto, ziwa na bahari zinaathiri propela na injini za meli na hivyo siyo tu kuhatarisha usalama wa vyombo hivyo, bali pia maisha ya abiria. Ni wajibu wetu kila mmoja kuzuia utupaji wa takataka ndani ya mito, maziwa na bahari,’’ amesema Sondo Maadhimisho ya siku ya mabaharia duniani hufanyika Juni 25 kila mwaka ambapo kwa Tanzania, wadau wa sekta ya usafirishaji kwa njia ya maji huadhimisha siku hiyo kwa kufanya maonyesho, kongamano na shughuli mbalimbali za elimu kwa umma kuhusu uhifadhi wa mazingira na usafirishaji salama majini.

Chanzo: Mwananchi