Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DIT yazindua mashine ya wagonjwa kupumua

DIT.jpeg DIT yazindua mashine ya wagonjwa kupumua

Tue, 7 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

TAASISI ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), imebuni mashine ya kumsaidia mgonjwa aliyeshindwa kupumua (ventilator), wakati huu wa uwapo wa ugonjwa wa virusi vya corona.

Mashine hiyo imebuniwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo hicho kwenye fani ya stashahada ya uhandisi vifaa tiba, kwamba wameitengeneza kwa muda wa miezi miwili.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana, mmoja wa wanafunzi hao, Inocent Dogras, alisema walilazimika kutengeneza kifaa hicho baada ya kutokea kwa mlipuko wa ugonjwa wa corona na kusababisha vifo vya watu wengi duniani.

“Baada ya kusikia kuwa Ventilator ni gharama kubwa kuinunua na wagonjwa wengi walikuwa wanafariki kwa kukosa kifaa hicho, hivyo tulilazimika kukitengeneza ili kuwasaidia wagonjwa hususani wanaoishi vijijini ambao hawana uwezo wa kumudu huduma za afya,” alisema Dogras.

Aliongeza kuwa DIT wamewapa msaada wa vifaa kwa ajili ya kutengeneza na kwamba kwa sasa hivi wameshakamilisha na kipo tayari kwa matumizi.

Mwanafunzi mwingine aliyeshiriki katika kutengeneza kifaa hicho, Aiche Rodgers, alisema kifaa hicho kazi yake ni kumsaidia mgonjwa kuingiza na kutoa hewa nje.

“Mgonjwa anapozidiwa kupumua tunamvalisha face mask ambayo kwa asilimia 80 hadi 90 inamsaidia kuingiza na kutoa hewa nje, alafu mashine hii (Ventilator) ndiyo itakayomsaidia kupumua vizuri kwa muda wote hadi atakapopona,” alisema Rodgers.

Ofisa uhusiano wa DIT, Amani Kakana, alisema uongozi wa chuo umewapa elimu ya ubunifu wanafunzi hao ambao umewawezesha kubuni kifaa hicho, kwamba lengo kuu la DIT ni kuhakikisha changamoto zilizopo katika jamii zinatatuliwa.

Kakana alisema baada ya kuingia kwa mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya corona ndipo lilipobuniwa wazo la kutengeneza mashine hiyo, baada ya kusikia kwamba kuna upungufu.

Alisema DIT iliwawezesha vifaa wanafunzi hao pamoja na fedha ili waweze kukamilisha ubunifu wa kifaa hicho ambacho hadi sasa kimeshakamilika kwa asilimia mia.

Kakana alisema: “Huwa tunatenga fedha kwa ajili ya miradi inayotatua changamoto katika jamii, hivyo kwa wahaa wanafunzi tuliwasilikiza mahitaji yao kasha sisi tukaenda kununua vifaa wanavyovihitaji.”

Alisema baada ya kukamilika kwa kifaa hicho wameshawasiliana na hospitali mbalimbali kama vile Aga Khan, Hospitali ya Rufani ya Amana, pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili tawi la Mloganzila kwa ajili ya kuanza kukitumia kifaa hicho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live