Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

DIT yajiapambanua hivi mapinduzi ya viwanda

Viwanda DIT DIT yajiapambanua hivi mapinduzi ya viwanda

Tue, 21 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dunia hivi sasa ipo kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda ambapo sifa yake kubwa ni matumizi makubwa ya teknolojia ya kidijiti katika uzalishaji na utoaji wa huduma za kijamii.

Mabadiliko hayo yana kasi kubwa ndio maana miaka michache iliyopita teknolojia zinazochipukia zilikuwa ni mada za majadiliano katika majukwaa ya sayansi, teknolojia na ubunifu kwenye eneo la akili bandia, matumizi ya roboti katika shughuli za uzalishaji, sayansi data na mtandao wa mawasiliano ya vifaa.

Hivi sasa matumizi ya teknolojia hizo yanachipukia katika sekta za fedha, elimu, usafirishaji, viwanda, kilimo na huduma za afya, teknolojia ambazo zimepata umaarufu mkubwa katika miaka ya hivi karibuni na ni moja ya ubunifu mkubwa uliofanyika katika karne ya 21.

Kutokana na hayo, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), imejipanga kuendesha mafunzo yake kiubunifu zaidi kwa kuhusisha mafunzo ya

kitaalamu, teknolojia atamizi na mafunzo kwa vitendo viwandani.

Mkuu wa DIT, Profesa Preksedis Ndomba anasema mafunzo ya kitaalamu yameimarishwa kwa kuendesha mitaala inayokidhi mahitaji ya soko na kuongeza bajeti ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kuwashirikisha wanafunzi katika kutatua changamoto za kiufundi zinazozikabili DIT kama vile uchakavu wa Miundombinu.

Anasema taasisi hiyo imeanza kutoa mafunzo ya vitendo viwandani kwa kuanzisha viwanda vidogo vya kufundishia hapo chuoni au kushirikiana na wamiliki wa viwanda halisi vya uzalishaji nje

ya chuo.

Profesa Ndomba anasema pamoja na mambo mengine taasisi hiyo imeingia mikataba 30 na taasisi na viwanda mbalimbali ndani na nje ya nchi ili kuwawezesha wanafunzi kutembelea na kushiriki kwenye mafunzo kwa vitendo kwenye viwanda husika.

Baadhi ya taasisi hizo zipo nchini Tanzania, Italia, China, Marekani, Ethiopia na Finland.

“Itoshe tu kusema kwamba kundi la wahitimu ambao wamemaliza mwaka huu, walipodahiliwa walikuta tayari taasisi yetu inasimamia utekelezaji wa mafunzo viwandani na ninashawishika kuamini kuwa dhana hii wameielewa vilivyo na kupitia dhana hiyo,” anasema.

Anasema kutokana na kuiva kwa wahitimu hao baadhi yao walishiriki katika kufanya mambo mbalimbali ya kuchangia katika kutatua changamoto mbalimbali katika taasisi hiyo kwa kutumia kampuni walizounda wakashindanishwa na hatimaye kukabidhiwa miradi kwa utekelezaji.

“Kipindi hicho cha Covid 19 katika kupambana na maambukizi hayo tulibuni na kutengeneza mashine ya kunawia mikono, mashine ya kusaidia kupumua kwa wagonjwa wenye changamoto ya upumuaji,

“Pia tumebuni, kutengeneza na kubiasharisha mashine mbalimbali kama vile mashine ya kutengeneza chakula cha samaki, mashine ya kuuza maziwa, mashine ya kuuza maji, utengenezaji wa spea mbalimbali kwa kutumia mashine ya 3D printing pamoja na kuatamia wabunifu mbalimbali,” anasema.

Pia anasema anatambua juhudi na kujituma kwa watumishi wa taasisi hiyo ambazo zimesababisha sherehe ya mahafali ya 15 kwa wahitimu 1004 wa mwaka huu kufana jijini Dar es Salaam. Naye Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi hiyo, Dk Richard Masika anasema DIT imejipambanua kuwa kiongozi katika kuchachua maendeleo ya viwanda kupitia ukuzaji wa teknolojia na ubunifu.

Anasema kama Baraza wamefanikiwa, kurasimisha Kampuni ya Teknolojia ya DIT yenye usajili wa BRELA ili kubiasharisha bunifu kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali za jamii katika fani za uhandisi na teknolojia nchini.

“Taasisi imepata msukumo mkubwa kutoka serikalini kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, kuiendeleza kampuni hiyo kwa lengo la kutekeleza azma ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda na utekelezaji wa dhana mpya ya ufundishaji ya kiwanda cha mafunzo,” anasema.

Anasema ili maendeleo endelevu ya viwanda yapatikane, kila moja anafahamu kuwa taifa linahitaji rasilimali watu wenye elimu bora na mahiri, hasa katika kada za ufundi sanifu na uhandisi.

“Kati ya kada nilizozitaja, mashirika ya maendeleo ya kimataifa yanapendekeza kuwa uwiano kwa kila mhandisi mmoja, mafundi sanifu watano na mafundi stadi 25 ili kuleta tija na ufanisi katika shughuli za uzalishaji hasa viwandani,” anasema.Anasema kuwa takwimu zilizopo zinaonesha kwamba uwiano huo haupo hapa nchini na hakuna dalili za kuukaribia kwani zikiangaliwa takwimu za wahitimu wa uhandisi zinalingana na zile za mafundi sanifu au wakati mwingine wahandisi wahitimu ni wengi kuliko wahitimu wa ufundi sanifu.

“Tatizo ni kubwa na linaendelea kuwa kubwa zaidi. Mfano halisi unadhihirishwa na takwimu za wahitimu hawa wa DIT wa mwaka huu ambao kati yao takribani asilimia 56 tu ndio mafundi sanifu,” anasema.

Anasema kwa kuzingatia hali hiyo, bila shaka huduma za ufundi na za kihandisi hazitakidhi mahitaji ya maendeleo yanayotarajiwa na huenda itakuwa vigumu kufikia malengo makuu ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa mwaka 2021/22 – 2025/26 kama hali hiyo itaachwa ienkama ilivyo.

Anasema kutokana na changamoto hiyo anaomba programu za ufundi sanifu zipewe kipaumbele katika mipango ya maendeleo hasa kutoa ufadhili kwa kundi maalumu la wanafunzi wa stashahada ya uhandisi ili kuvutia wanafunzi kujiunga kwa wingi na vilevile kuvutia vyuo kuongeza idadi ya wanafunzi hao.

“DIT imepanga kuongeza idadi ya wanafunzi wa ufundi sanifu uhandisi kwa zaidi ya asilimia 50 ya waliodahiliwa hivi sasa iwapo itapata nafasi ya kupanuka kwa haraka,” anasema. Anasema mafunzo ya ufundi ama uhandisi hukamilika vizuri zaidi kwa wanafunzi kushiriki mafunzo kwa vitendo Chuoni na viwandani, lakini kumekuwa na utayari mdogo wa viwanda kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.

Pia nafasi za wahadhiri wa taasisi hiyo kujifunza kwa vitendo viwandani ni finyu pamoja na utayari wa wataalamu wa viwandani kujitolea kutoa uzoefu wao katika taasisi hiyo ni mdogo.

“Tunaomba serikali ishawishi viwanda kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo na kuruhusu wataalamu wao kufundisha vyuoni kwa kujitolea au hata kwa malipo kidogo,” anasema.

Anawashauri wahitimu kutumia akili na maarifa waliyoyapata zaidi ya vile wanavyotumia Apps au simu zao. “Mfano, ukitumia Apps au ukicheza na simu mara moja basi fanya kazi mara kumi au zaidi,” anasema.

Katika mahafali ya 15 ya DIT, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako alisema taasisi hiyo ina wajibu mkubwa katika kutekeleza azma ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda kwani ina wataalamu wa kutosha katika sekta ya fundi.

Ndalichako alisema ni vigumu kutenganisha sayansi, teknolojia na ubunifu na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi. Hivyo akasema ni jukumu la watafiti, wabunifu na wavumbuzi katika sekta zote kuchukua hatua za makusudi kubuni na kutumia teknolojia zinazochipukia kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi.

MWANZO MWISHO

“Jambo la msingi kwetu sisi kama nchi, ni kuendelea kufanya utafiti na kuona namna ambavyo teknolojia hizo zinaweza kutumiwa kutatua changamoto zinazoikabili jamii na kwa manufaa ya kiuchumi,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live